Image
Image

Niyonzima ameomba radhi wanachama, viongozi na mashabiki wa yanga.

KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima ameomba radhi wanachama, viongozi na mashabiki wa klabu hiyo, kufuatia mambo yaliyotokea dhidi yake na kusababisha kuvunjiwa mkataba kwa utovu wa nidhamu.
Mwishoni mwa mwaka jana, Yanga ilitangaza kuvunja mkataba na mchezaji huyo kwa utovu wa nidhamu baada ya kuchelewa kuripoti kwenye kambi ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania baada ya kumalizika kwa michezo ya Chalenji nchini Ethiopia alikokuwa akitumikia timu yake ya taifa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari kwenye ofisi za klabu ya Yanga, Niyonzima alikiri kufanya makosa na kuomba msamaha kwa wale aliowakosea, lakini pia kuwasamehe waliomkera na kuahidi mashabiki na wanachama kuwa mambo yamekwisha kwani kilichobaki ni kuangalia mbele.
“Nilipata matatizo na klabu yangu lakini hayakuwa makubwa kama ambavyo watu hufikiria, nashukuru tumeweza kukaa na uongozi na kuweza kuyatatua na mpaka sasa tuko hapa, yamefikia pazuri na najua tutaendelea kufanya kazi,” alisema.
Alisema Yanga ina haki ya kulalamika juu ya kile alichokifanya kwani alivyokwenda nyumbani kwao kuitumikia timu yake ya taifa alikuwa na maumivu yaliyomfanya kujitibia mwenyewe huku akikiri wazi hakukuwa na mawasiliano ambayo yalisababisha yote yatokee.
Alisema: “Kikubwa ni kwamba nilikaa na viongozi wangu na kuyazungumzia, kuangalia ni wapi nimekosea mimi kama binadamu, na kufikia pazuri,” alisema.
Niyonzima alisema alishtushwa na uamuzi ambao ulichukuliwa na klabu hiyo, kwani hakutarajia kitu kama hicho kingetokea. Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema Niyonzima ni mtoto kwao hivyo ana imani msamaha wake utachukuliwa na wanachama na viongozi wa Yanga na kuufanyia kazi.
Alisema uongozi wa klabu yake unajipanga kutoa taarifa rasmi kuhusu suala la Niyonzima ambayo itahitimisha mjadala mzima.
“Kwetu sisi Niyonzima ni mtoto, na siku zote mtoto anapokuja kwako akaunyea mkono haukatwi, unaupangusa na natumaini mashabiki, wapenzi wa Niyonzima watamsikia alichokisema na viongozi wetu wamesikia aliyosema, kwa hiyo sisi kama Yanga tumeyapokea kwa mikono miwili, tutayafanyia kazi,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Sisi kama uongozi wa Yanga, tunamshukuru Niyonzima kwa kuwa muungwana juu ya hili suala na kuamua kuja kwa uongozi wa Yanga na kuomba radhi kwa yote yaliyotokea, tutatafakari kwa manufaa ya klabu na kutoa majibu, ” alisema.
Uongozi wa Yanga ulifikia hatua ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo kufuatia kurudia makosa mara nyingi, kiasi cha kuikera klabu yake na kuamua kumchukulia hatua hiyo sambamba na kutakiwa kuilipa klabu hiyo zaidi ya dola za Marekani 71,175 kama fidia inayotokana na mkataba mpya unaomalizika 2017.
Ingawa suala hilo halijawekwa wazi bado, lakini habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa mchezaji huyo amerudishwa kundini na huenda akajiunga na wenzake wiki hii.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment