Image
Image

Kwa pamoja tumpe nguvu Rais Magufuli atekeleze ndoto aliyonayo kwa Tanzania.

KATIKA salamu zake za Pasaka kwa Watanzania, Rais John Magufuli amewataka Watanzania kuendeleza upendo na mshikamano walionao ili kuendelea kuilinda amani ya nchi na wasibaguane.
Salamu hizo alizozitoa juzi kwenye Ibada ya Pasaka, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front, Dar es Salaam, ziwe dira na mwongozo mpya kwa Tanzania tuitakayo. Kwa msisitizo, Rais Magufuli alisema Watanzania wanapaswa kutokubaguana kwa dini, rangi wala makabila na washirikiane katika umoja wao.
Akaongeza kwamba wakati taifa likiadhimisha sikukuu hiyo ya kufufuka kwa Yesu Kristo, wananchi wanapaswa kusherehekea kwa kufanya kazi ili taifa lisonge mbele. Akasema sikukuu hiyo ya kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo, Watanzania wafufuke naye katika upendo wake, lakini pia wahakikishe wanafanya kazi kweli kweli kwa sababu vitabu vinasema ‘asiyefanya kazi na asile’.
Akabainisha kwamba endapo Watanzania kwa umoja wao, wakiamua kufanya kazi kwa bidii, Taifa halitakuwa masikini na kuacha kutegemea misaada ya wahisani wa nje. Tunaungana na Rais katika kauli zake, zinazosisitiza upendo, mshikamano na bidii ya kazi, kwani vikiwa ndiyo dira ya nchi, tutasonga mbele na kusahau umasikini uliotesa taifa hili kwa muda mrefu.
Rais Magufuli anasema Tanzania ni nchi iliyojaaliwa neema kwa kuwa na rasilimali nyingi na hivyo wananchi wanatakiwa kusimama imara ili iweze kuja kuwa Taifa litakalokuwa likitoa misaada kwa mataifa mengine ya nje.
Ni ukweli usiopingika kwamba misaada mara nyingi huambatana na masharti, na nchi hii inao uwezo wa kuwa na bajeti bila kutegemea misaada, ilimradi watu wake wafanye kazi na waifanye kwa bidii na maarifa.
Uwezo huo tunao, nia ipo na sababu ya kufanya hivyo tunayo. Rais anaamini Tanzania bila misaada, inawezekana na Watanzania waliwezeshe hilo. Taifa hili linahitaji kurudisha uzalendo.
Tukane ubinafsi, ufisadi, rushwa, upendeleo, uzembe, udini, ukabila na mengine ya namna hiyo, ambayo yamelifanya taifa liwe tegemezi huku rasilimali zikiibwa mchana kweupe kwa ajili ya watu wachache waliokabidhiwa nyadhifa wakazitumia vibaya kwa faida yao.
Kama salamu alizotoa Rais Magufuli zinafanyiwa kazi, imani yetu ni kwamba tutaondokana na utegemezi, tutakuwa na bajeti inayotokana na makusanyo ya ndani na tutaachana na kutegemea mataifa makubwa ambayo nayo yameendelea kwa sababu ya umoja wao na kuchapa kazi kwa bidii na maarifa.
Rais Magufuli pia akawaomba Watanzania, kutochoka kuliombea Taifa pamoja na yeye ambaye ana jukumu gumu na zito, lakini kupitia maombi ya wananchi anaamini atatimiza yale aliyotakiwa kuyatimiza.
Katika hili, tunaamini kila Mtanzania kwa imani yake, ana wajibu wa kuliombea taifa na Rais Magufuli ili vita anayopigana aweze kuishinda. Tuungane pia na Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliyeongoza ibada hiyo ambaye aliwakumbusha wananchi, kurejesha maadili kwa kumrudia Mungu.

Askofu Malasusa pia akawataka Watanzania kwa imani zao, kuacha kumsifu Rais Magufuli kwa kupiga makofi na badala yake kila mmoja kwa imani yake, asimame na kumuombea kwa kuwa sasa taifa limeanza kuwa na matumaini mapya na nuru kwa kumpata kiongozi aliye mwadilifu. Imani yetu ni kwamba Watanzania wamesikia na wako tayari kuenzi salamu hizi muhimu ili taifa liweze kusonga mbele.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment