Image
Image

Mamia wauaga mwili wa dada wa bilionea Msuya



Anethe, ambaye ni mdogo wa mfanyabiashara maarufu, bilionea Erasto Msuya (naye marehemu), aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi.
Katika ibada ya kuaga mwili huo, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Salasala, mtoto wa marehemu, Allen Kimario, aligoma kuaga mwili wa mama yake.
Baada watu mbalimbali kumaliza kuaga mwili huo, ilifika zamu ya ndugu kuaga ambao walikuwa wameambatana na mtoto huyo, aliyekuwa ameshikiliwa mikono.
Mtoto huyo aligoma hivyo kuwafanya ndugu kufanya kazi ya ziada kumlazimisha kuuaga mwili wa mama yake kwa kumnyanyua, lakini hakukubali hivyo kupita mbele ya jeneza akiwa ameangalia pembeni. Muda wote wa ibada, Allen alikuwa ameshikilia picha ya mama yake hata wakati wa kuaga.
Awali, majirani waliokuwa wakiishi na marehemu, walisimulia mtoto huyo alivyopata shida baada ya mama yake kuuawa.
Zuhura Ali, mmoja wa majirani hao, alisema asubuhi ya Alhamisi, baada ya tukio hilo kutokea usiku wake, walishangaa mtoto anakwenda nyumbani kwao huku akiwa amevalia nguo za shule na kuwaomba waende wakamsaidie kumwamsha mama yake.
Alisema walishanga kuambiwa hivyo na kulazimika kumfuata hadi nyumbani. Alisema walipofika walianza kumwita mama yake, lakini mtoto huyo aliwaambia kwamba mama yake hawezi kuitika, hivyo kulazimika kuingia ndani.
Zuhura alisema baada ya kuingia, walikuta Anethe akiwa amelala chini huku mwili wake ukionekana kutapakaa damu hivyo kuwaita watu wengine na kuanza kusaidiana kutoa taarifa katika vyombo husika.
“Sijaamini kitu ambacho kimemtokea Anethe. Alikuwa jirani na rafiki yangu. Tulikuwa tunatembeleana na wakati mwingine kama mimi niko kwangu na yeye ameketi kibarazani kwake alikuwa ananipungia mkono au kunipigia simu akinijulisha kwamba ananiona kwa sababu ukuta wangu ni mfupi kwa hiyo ni rahisi kuniona. Ninasikitika na itanichukua muda mrefu kumsahau,” alisema.
Baba mdogo wa marehemu, Ombeni Msuya, alisema pamoja na kwamba familia yao inaandamwa, hawataogopa bali wataendendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu.
Alisema wanaamini vyombo vya dola vitafanya kazi yake ili kubaini kilicho nyuma ya tukio hilo na kwamba mazishi ya mwanawe yanatarajia kufanyika leo Mererani, Simanjiro mkoani Manyara.
Alisema Anethe alikuwa na mchango mkubwa katika familia yao na kwamba ameacha mtoto mmoja.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ambako Anethe alikuwa anafanya kazi, Geofrey Mponda, alisema Anethe, alikuwa msada mkubwa katika ofisi yao na wamepoteza mfanyakazi muhimu katika Idara ya Uchumi.
Alisema hadi mauti yanamkuta alikuwa mchumi daraja la pili na alikuwa akifanya kazi katika Idara ya Uchambuzi wa Sera.
Kwa mujibu wa watu wa karibu, baadhi ya ndugu wa familia hiyo wamekuwa wakifariki katika aina ya vifo vya kufanana kikiwamo cha bilionea Erasto Msuya aliyeuawa kwa kufyatuliwa risasi Julai 7, mwaka 2013 eneo la Mijohoroni, kando ya barabara ya Arusha na Moshi, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment