Image
Image

Kukutana Lowassa, Magufuli iwe chanzo kudumisha amani



KUKUTANA kwa mara ya kwanza kwa Rais John Magufuli na aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa jijini Dar es Salam jana kumeleta msisimko na faraja ya aina yake kwa watu wanaofuatulia kwa karibu maendeleo ya siasa za Tanzania.
Tukio hilo la aina yake, na ambalo ni la kwanza kutokea tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25 uliomuweka madarakani Rais Magufuli aliytegombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni habari njema kwa walio wengi kwa sababu wawili hao hawakuwahi kukutana katika tukio lolote lile hapo kabla.
Lilitokea katika maadhimisho maalumu ya sherehe za kutimiza miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na kushuhudiwa na viongozi wengine mbalimbali wastaafu wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya Joseph Warioba. Alikuwapo pia njane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere.
Kukutana kwa Rais Magufuli na Lowassa katika tukio hilo, ndiko kulikotusukuma na kuona kwamba sasa, kuna kila sababu ya Watanzania wote kujifunza kupitia tukio hilo, kwamba siasa siyo uadui hata kidogo.
Sisi, Nipashe, tunajua kwamba jambo hilo ni la kawaida kwa Watanzania. Kwamba, mara zote, ushindani wa kisiasa huwa hauchukuliwi kuwa chanzo cha watu kuhasimiana. Ni tabia iliyodumishwa kwa miaka mingi na mara zote inapaswa kuendelezwa kwa nia ya kudumisha amani, utulivu na Tanzania iliyo moja.
Tumeshawishika kugusia tukio la kukutana kwa Lowassa na Magufuli, ambao walishikana mikono na kuketi pamoja huku muda wote wakionyesha nyuso za tabasamu, kuwa ni funzo kwa kila mmoja katika kudumisha imani.
Zipo sababu za sisi kukumbushia jambo hili. Ni kwamba, baada ya kumalizika kwa uchaguzi, wapo baadhi ya Watanzania ambao bado wangali wakisuguana kiitikadi katika namna ya kutishia amani na utulivu.
Inakumbukwa kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita, Magufuli alitangazwa mshindi baada ya kuvuna zaidi ya asilimia 58 ya kura halali zilizopigwa.
Aidha, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uxhaguzi (NEC), Lowassa, ambaye aliwakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akishika nafasi ya pili baada ya kupata zaidi ya asilimia 39 ya kura hizo. Matokeo hayo yaliwafurahisha wengi na pia kuwasononesha baadhi yao.
Lowassa na vyama vinavyomuunga mkono havikuridhishwa kutokana na baadhi ya mambo yalivyokuwa. Hata hivyo, wapinzani wote, akiwamo Lowassa, walisema kuwa wanalazimika kumtambua Rais Magufuli kwa nia ya kudumisha amani huku wakijipanga zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Pamoja na yote, hivi karibuni pametokea msuguano wa aina nyingine. Baadhi ya vyama vya upinzani, ikiwamo Chadema ya Lowassa, haikubaliani na baadhi ya maamuzi ya Serikali ya Rais Magufuli kuhusiana na mwenendo wa siasa nchini. Ni kupitia mvutano huo, ndipo kukaibuka msuguano juu ya kufanyika kwa mikutani na maandamano ifikapo Septemba Mosi.
Hali ya hofu imekuwa ikitamalaki kwa baadhi ya wananchi kuhusiana na msuguano unaoendelea baina ya pande mbili, yaani Chadema ya Lowassa na vyombo vya dola. Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa kukutana huko kwa Magufuli na Lowassa jana ni ishara njema kuwa amani itaendelea kudumishwa kama ilivyo kwa desturi ya Watanzania walio wengi.
Kwamba, hata kama Magufuli na Lowassa hawakupata fursa ya kuzungumzia lolote kuhusiana na mvutano wa kauli za kisiasa unaoendelea, lakini ni wazi kwamba kushikana kwao mikono na kuzungumza kwa bashasha ni ishara njema ya kudumu kwa amani nchini.


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment