Image
Image

Profesa Ibrahim Lipumba, kimbunga kinachopita CUF

                                               Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.
MWANASIASA mkongwe nchini, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, mwaka 1995 alimuita Augustine Mrema kuwa ni kimbunga.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la Pili ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, kimbunga ni upepo wenye nvuvu nyingi, tufani, halibari, dhoruba.
Mzee Kingunge alitoa kauli hiyo akiwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiongoza Idara ya Itikadi na Uenezi.
Alikuwa akitoa kauli ya chama hicho, baada ya kada wake aliyekuwa na ushawishi mkubwa, Augustine Mrema, kutangaza kujitoa CCM, na kujiunga na NCCR-Mageuzi.
Katika kufafanua kauli hiyo, Kingunge alikiri kwamba Mrema ni mwanasiasa mwenye ushawishi, na kwamba CCM ilitikiswa na kujiondoa kwake, lakini tukio hilo ni kimbunga kinachopita na baadaye mwanasiasa huyo atasahaulika na chama kitaendelea kuwa na umaarufu wake.
Utabiri wa Kingunge ulithibitika, kwa kuwa umaarufu wa Mrema ulipanda ghafla kisha kuporomoka taratibu.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 1995, Mrema aliyegombea kupitia NCCR-Mageuzi alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,808,616, nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM, ambaye alipata kura 4,026,422 .
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Mrema aliporomoka hadi nafasi ya tatu.
Rais Mkapa alipata asilimia 71.74 ya kura zote za Urais 5,863,201 wakati Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF), akipata asilimia 16.26 sawa na kura 1,329,077, wakati Mrema akigombea mara ya pili kupitia Tanzania Labour Party (TLP), alikohamia mwaka 1999, akipata kura 637,077.
Hili lilikuwa poromoko kubwa kwa Mrema la kura 1,171,539 ndani ya miaka mitano kutoka mwaka 1995 hadi 2000.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, kimbunga cha Mrema kikaisha kabisa kutokana na kushika nafasi ya nne kwa kupata kura 84,901 (asilimia 0.75), nyuma ya Jakaya Kikwete aliyepata kura 9,123,952 (asilimia 80.28) Prof. Lipumba kura 1,327,125 na Freeman Mbowe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kura 668, 756.
Nilitumia takwimu hizi kuonyesha kwamba utabiri wa Kingunge dhidi ya Mrema ulikuwa wa kweli katika ulingo wa sisasa, kwa kuwa hakugombea tena urais zaidi ya kugombea ubunge wa Vunjo 2010 na kushinda, lakini mwaka jana alipoteza kwa James Mbatia, hivyo kwa sasa hana nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa.
Chama cha CUF, kimeingia katika mgogoro na Mwenyekiti wake wa zamani, Profesa Nguyuru Ibrahim Haruna Lipumba, ambaye aliandika barua ya kujiuzulu Agosti, 2015.
Lipumba alichukua uamuzi huo kutokana na kutokubaliana na uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpokea Edward Lowassa na kumsimamisha kuwa mgombea urais.
Prof. Lipumba hivi karibuni alitangaza kuandika barua ya kutengua barua ya awali ya kujiuzulu na kutaka kuwania kiti hicho katika uchaguzi ulioitishwa Agosti 21.
Hata hivyo, jina lake halikupitishwa, hali iliyozua vurugu siku ya uchaguzi, baada ya kutokea akiwa na wafuasi wake wakishinikiza aruhusiwe kugombea.
Vurugu hizo zilivunja mkutano huo kabla ya uchaguzi, ingawa wajumbe wengi walishapiga kura ya kumkatalia.
Maneno mengi yanasemwa kuhusu msomi huyo mbobezi wa uchumi.
Baadhi ya watu wanasema ndiye anayestahili kuwa mwenyekiti wa CUF, na wengine wanasema hatua yake ya kujiuzulu, tena katika mazingira tata inampotezea sifa ya kuaminika kama kiongozi mkuu wa chama kikubwa, kama CUF.
Binafsi namuona Lipumba kama kiongozi mpambanaji na aliyetumia muda wake mwingi kuhamasisha uhai wa CUF, kwa upande wa Tanzania Bara tangu ashike nafasi ya uenyekiti mwaka 1995.
Hata hivyo, kasi ya CUF kustawi kwa maana ya kuwa na wanachama na wafuasi wengi kwa upande wa bara imekuwa ndogo kwa kipindi cha uongozi wake wa miaka 20 kulinganisha na Chadema.
Kwa kipindi chote hicho ukiacha Zanzibar, CUF imekuwa na ngome ya wafuasi katika mikoa ya Mtwara na Lindi tu, ingawa uchaguzi uliofanyika bila Prof. Lipumba kuwapo, ndipo ilipata viti sita ambavyo ni vingi katika mikoa hiyo kulinganisha na miaka iliyopita.
Wakati wa uongozi wa Lipumba, CUF Dar es Salaam, iliwahi kupata mbunge mmoja tu, Frank Magoba (Kigamboni).
Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka jana ilipata majimbo mawili ya Kinondoni na Temeke na kuyakosa kwa bahati mbaya ya Segerea na Mbagala.
Jimbo ambalo pia CUF ililipata Bara mwaka jana ni la Kaliua, ambalo linashikiliwa na Magdalena Sakaya, ambaye hata hivyo, juzi alisimamishwa uanachama.
Kimsingi, fursa ya CUF kufanya vizuri zaidi na kupata viti tisa vya ubunge Bara mwaka jana ilitokana na ushirikiano wa Ukawa, na siyo mchango wa Prof. Lipumba katika kuhamasisha shughuli za chama hicho.
Profesa Lipumba kwa takribani miaka 10 ya uongozi wake kwa CUF, inatosha na mchango wake unapaswa kuheshimika na kuenziwa wakati damu mpya ikisubiriwa kupokea kijiti chake kama alivyompokea marehemu Mageni Musobi, ambaye naye alipokea kijiti cha Mzee James Mapalala.
Kupumzika katika uongozi ni jambo la msingi na lenye busara na heshima, hata kama wanachama au wananchi bado wanakupenda kuliko kukuchoka.
Hatua ya Prof. Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu uongozi na kutangaza kwamba atabakia kuwa mwanachama mtiifu ulikuwa ni uamuzi uliopaswa kuheshimiwa na uongozi na wanachama wote wa CUF.
Kiongozi aliyekomaa anapofanya uamuzi bila kulazimishwa wala kushurutishwa kama alivyofanya Prof. Lipumba mwaka jana, alipaswa auheshimu yeye binafsi na ndiyo maana kwa upande mwingine, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, hakuijibu barua hiyo.
Maalim Seif alifanya hivyo pengine kutokana na mazingira ambayo Prof. Lipumba alifanya uamuzi huo alioutangaza kwa waandishi wa habari badala ya vikao halali vya CUF.
Kubwa ambalo lilionekana kutowafurahisha wafuasi wa CUF, ni Lipumba kujiuzulu wakati mchakato wa uchaguzi mkuu ukiwa umeanza, hali iliyosababisha hisia kuwa alifanya hivyo kukikomoa chama.
Kama nilivyoeleza awali kuhusu kimbunga, Prof. Lipumba naye ni kimbunga ndani ya CUF, kwa kuwa ameshaanza kusababisha mtikisiko, lakini baadaye kimbunga hicho kitapita chama hicho kitatulia.
Mwaka 2000, kuna kundi liliibuka ndani ya CUF likijiita Kamati maalum ya Kufufua CUF Bara, lililoongozwa na Michael Nyaruba na Jamaton Magodi, na kusema kweli lilikitikisa sana chama hicho, lakini baadaye lilipotelea kusikojulikana hadi leo.
Jaribio lingine kubwa la kuitikisha CUF, ni kitendo cha mmoja wa waanzilishi wake, Hamad Rashid Mohamed, kutaka Maalim Seif ajivue wadhifa wa katibu mkuu, kwa madai kuwa asingeweza kufanya kazi mbili kwa ufanisi na ya makamu wa kwanza wa rais katika iliyokuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Hamad Rashid aliwatikisa, lakini mwishowe aliamua kuanzisha chama chake cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Katika minyukano hii yote, Prof. Lipumba alikuwa miongoni mwa viongozi waliosimama kupambana na kina Nyaruba na Hamad Rashid, ambao waliitwa kuwa ni wasaliti.
Takwimu pia zinaonyesha kuwa umaarufu wa Prof. Lipumba umekuwa ukiporomoka katika uchaguzi wa urais kuanzia mwaka 1995 hadi 2010.
Kwa kuweka rekodi sawa, mwaka 1995 alishika nafasi ya tatu
Mwaka 2000, kura zake ziliongezeka kwa kupata 1,329,077 na kushika nafasi ya pili.
Mwaka 2005, kura zilishuka hadi 1,327,125 licha ya kushika nafasi ya pili na mwaka 2010 alizidi kuporomoka kwa kupata kura takribani 554,670 na kushika nafasi ya tatu.
Nimalizie kwa kusema kuwa kwa kuwa Prof. Lipumba ni mtaalamu wa uchumi, anapaswa kutumia fursa hiyo kufanya shughuli za kufundisha katika vyuo vikuu, utafiti na ushauri kama alivyoeleza alipokutana na waandishi wa habari kutangaza hatua yake ya kujiuzulu uenyekiti mwaka jana.
Nipashe.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment