Image
Image

Yanga imeivaa yaidungua 3-0 African Lyon Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

WENYE nyumba wamerudi! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana kuanza vizuri kampeni zao kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Yanga imeanza kutetea taji lake baada ya kutupwa nje ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa na TP Mazembe ya Congo DR mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya makundi.
Ikicheza soka safi, Yanga iliichukua dakika 19 kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Deus Kaseke baada ya kuunganisha pasi safi ya Simon Msuva.
African Lyon ambayo mechi ya kwanza ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam, jana ilizidiwa karibu kila idara na kuonekana kuchoka hasa katika kipindi cha pili. Msuva aliiandikia Yanga bao la pili katika dakika ya 59 akiunganisha pasi ya Haruna Niyonzima kabla ya kumpiga chenga kipa wa Lyon na kuujaza mpira wavuni.
Pamoja na kuelemewa huko, Lyon walijaribu kufanya mashambulizi ambapo katika dakika ya 76 Tito Okello alishindwa kumalizia mpira wa krosi akiwa amebaki peke yake na kipa.
Yanga iliendeleza mashambulizi na dakika ya 90, Amisi Tambwe alikosa bao baada ya mpira wa kichwa aliopiga kugonga mwamba na mpira kurudi uwanjani.
Zikiwa zimebaki sekunde chache mpira kumalizika, Juma Mahadhi aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Msuva aliandika bao la tatu kwa Yanga baada ya kazi nzuri ya Niyonzima.
Yanga itacheza mechi ya pili keshokutwa ambapo itamenyana na JKT Ruvu kwenye uwanja huohuo wa Taifa.
Kutoka kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Alexander Sanga anaripoti kuwa wenyeji Toto Africans wameshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbeya City.
Wageni Mbeya waliandika bao hilo katika dakika ya tano lililofungwa na Haruna Shamte kwa mpira wa adhabu iliyokwenda moja kwa moja golini.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment