Image
Image

Ushahidi kesi ‘scorpion’ ulivyoliza watu kortini




HALI ya mshtuko na simanzi ilitawala miongoni mwa watu waliofika kwenye Mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam jana kusikiliza kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, baada ya shahidi namba moja aliyedai kujeruhiwa mwilini, kuonyesha majeraha yake na namna alivyotobolewa macho hayo.

Inadaiwa kuwa shahidi huyo, Said Ally alijeruhiwa na kutolewa macho na Salum Njwete (34) maarufu ‘Scorpion’ Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni jijini Dar es Salaam.
Shahidi huyo alifika katika viunga vya mahakama hiyo majira ya saa mbili asubuhi tayari kwa kutoa ushahidi wa namna alivyodhuriwa.
Njwete aliwasili Mahakamani hapo saa 3:30 asubuhi akiwa kwenye gari maalumu la Jeshi la Magereza akisindikizwa na askari watano na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha mashtaka.
Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu Flora Haule, ilichukua muda wa saa 2:57 kwa Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga na Wakili wa Mshtakiwa, Juma Nassoro, kumuuliza maswali shahidi Ally.
Watu walifurika katika chumba cha mahakama hiyo hadi madirishani kusikiliza kesi hiyo ambayo tukio lake lilitikisa jiji la Dar es Salaam.
Mahojiano baina ya Wakili wa Serikali, Katuga na shahidi wa kwanza, Ally ambaye ndiye anayedaiwa kutobolewa macho na Njwete yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Septemba 6, mwaka huu, siku hiyo unakumbuka nini kuanzia majira ya asubuhi hadi jioni?
Shahidi: Niliamka saa moja asubuhi, nikaenda ofisini kwangu saa 2:30 asubuhi, nilifanya kazi siku nzima hadi saa nne usiku nilipofunga saluni.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya kufunga, nikaenda kituoni na kusubiria daladala na ilikuwa saa 4:20 usiku na ilipita bajaji, ikasimama, dereva aliniuliza unaenda wapi? Unaenda Buguruni? Nikamjibu siendi huku, akaniuliza tena unaenda wapi? Nikamjibu naenda Ubungo, akaniambia basi twende nikakuache Tabata Relini, nikapanda.
Wakili: Wakati unapanda mlikuwa watu wangapi?
Shahidi: Nilikuwa mimi na dereva tu. Na tulipofika Tabata Barakuda, dereva alikunja kulia nikamuuliza unaenda wapi huko mimi siendi huko. Dereva yule alinijibu "njia ya huko ni mbali tupite njia ya huku. Ukizingatia sina mafuta mengi". Na mimi nikamkubalia.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Alinifikisha Buguruni na nikamlipa Sh. 1,000.
Wakili: Ilikuwa saa ngapi muda huo?
Shahidi: Ilikuwa saa 4:40 usiku.
Wakili: Kwa muda huo Buguruni hali ilikuwaje?
Shahidi: Wafanyabiashara walikuwa wengi sana, hali iliyonivutia kununua kuku kwa ajili ya kuipelekea familia yangu, na nikaanza kutafuta sehemu wanapouza kuku.
Wakili: Kwa usiku huo uliwezaje kuona sehemu wanapouza kuku?
Shahidi: Kulikuwa na taa za wafanyabiashara na taa za barabarani.
Wakili: Taa za wafanyabiashara zikoje?
Shahidi: Ni taa za balbu zilizokuwa zimening’inizwa kwa nyaya.
Wakili: Endelea
Shahidi: Nikachagua kuku, nikamuuliza yule muuzaji kuku Sh. ngapi? Naye akanijibu ni Sh. 7,000, nikaomba anipunguzie na aniuzie kwa Sh. 6,000, baada ya hapo nilimpa Sh. 11,000 ilikuwa ni noti ya Sh. 10,000 na noti ya Sh. 1,000 ili anipatie Sh. 5,000.
Wakili: Huyo muuza kuku ni jinsia gani?

Shahidi: Wa kiume mwembamba na alikuwa amevaa cheni shingoni.
Wakili: Yeye alisemaje?

Shahidi: Akasema kuku ni Sh. 6,500, na wakati nabembeleza bei ya kuku, kuna kijana mmoja alikuja kusimama upande wangu wa kulia katika bega langu la kulia, akasema 'brother' (kaka) nina shida naomba unisaidie. Nikamjibu "unashida gani? Kama nitaweza kukusaidia nitakusaidia kama sitaweza kukusaidia basi."
Wakili: Je, wakati unamjibu ulimtazama?
Shahidi: Ndiyo nilimtazama.
Wakili: Je, umegeuka kumtazama ieleze mahakama ulikuwa unamfahamu?
Shahidi: Hapana, nilikuwa simjui na sikuwahi kufika eneo hilo, nilipata shaka kidogo, nilimwambia muuza kuku, asimbabue kuku kwa sababu naenda kumweka katika friji, huyo mtu aliyesimama nyuma yangu alikuwa amevaa kibegi kiunoni na alikuwa anakifungua, nikaja kushtuka nimechomwa kisu bega la kushoto.
Wakili: Ulichomwa hicho kisu na mtu gani?
Shahidi: Na huyo huyo aliyesimama nyuma yangu.
Wakili: Toka wakati amesimama nyuma yako hadi anakuchoma, ilichukua muda gani?
Shahidi: Haikuchukua hata dakika mbili na nilichomwa visu vya haraka haraka.
Wakili: Uliwezaje kumwona mtu huyo wakati ulikuwa ni usiku?
Shahidi: Kulikuwa na taa, mwanga mkubwa sana wa magari na taa za barabarani.
Wakili: Hilo eneo ni hatua ngapi hadi kituoni?
Shahidi: Kama hatua 10 hadi kituoni.
Wakili: Alipokuchoma kisu, ukafanya nini?
Shahidi: Nilipiga kelele kuomba msaada, naye akasema hakuna wa kukusaidia, nilichomwa visu vinne tumboni nikaanguka chini, baada ya hapo nikasikia mmoja wa wauza chipsi akisema “Scorpion umeshaua” akaniacha, akaanza kunisachi mifukoni akachukua vocha na Sh. 21,000 nilizokuwa zimezishika mkono wa kushoto, na kwenye pochi kulikuwa na Sh. 300,000, akachukua na cheni ya silva niliyokuwa nimevaa shingoni na mkononi.
Wakili: Wakati anakata cheni, ulifanya nini?
Shahidi: Nilipiga kelele hadi nikachoka, cheni yangu ya shingoni ilkuwa na thamani ya Sh. 60,000 na ya mkononi Sh. 85,000.
Wakili: Halafu ukafanya nini tena baada ya hapo?

Shahidi: Nilikaa kimya tu nikimtizama, akawa anachukua simu zangu ndipo nilipomsikia mmoja wa wauza chipsi akisema ‘Brother' Salum mwachie simu zake ili aweze kuwasiliana na ndugu zake wajue kama yupo hapo.
Wakili: Alipoambiwa hivyo, nini kiliendelea?
Shahidi: Nikaona akimpiga teke huyo kijana kisha akanirudia mimi na kunivua fulana yangu.
Wakili: Wakati anakuvua T-shirt yako, uwezo wako wa kuona ulikuwaje?
Shahidi: Nilikuwa naona na akawa ananivutia barabarani.
Wakili: Wakati anakuvuta, ukawa unafanya nini?
Shahidi: Nilikaa tu, akaniweka barabarani, gari moja lilisimama karibia yangu, nikamsikia mtu huyo akisema "mgonge tu".
Wakili: Ilichukua muda gani?

Shahidi: Kama dakika nne hivi.
Wakili: 'Okay', Buguruni ni 'Double road' (njia mbili) ulikuwa barabara ipi? Iliyokuwa inaelekea Ubungo?
Shahidi: Karibia na kona ya barabara ya magari yanayotokea Buguruni kuelekea Ubungo, ni kama hatua tatu kufika mataa.
Wakili: Je, gari lilikugonga?

Shahidi: Hapana, gari lilirudi nyuma likanikwepa na kuondoka, ilipita kama dakika 30, akanivuta na kunipeleka pembezoni mwa barabara.
Wakili: Alikuwa anakueleza nini?
Shahidi: Alikuwa hasemi kitu.
Wakili: Endelea... baada ya hapo, nini kilifuata?
Shahidi: Akanichoma na kisu jicho langu la kushoto na nikazimia hapo hapo, nikakata mawasiliano, nikapata fahamu akaja msamalia mwema aliniuliza "una simu?"
Wakili: Hiyo sauti iliyokuuliza ilikuwaje?
Shahidi: Ilikuwa tofauti na ile ya mwanzo na ilikuwa ni jinsia ya kike, nikatoa simu nikampa naye akampigia simu mke wangu ambaye naye akampigia simu mdogo wangu.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Huyo mtu aliniuliza unaweza kupanda gari? Nikamjibu ndiyo naweza lakini sioni.
Wakili: Unasema mpaka sasa unaona giza?

Shahidi: Ndiyo hata hapa sioni kitu.
Wakili: Wakati anakutendea kitendo hicho, ulikuwa unaona? Je, unaweza kumtambua kwa wajihi kwa kuielezea mahakama ni mtu wa aina gani?
Shahidi: Ninaweza kwa sababu ninamshukuru Mungu wakati ameniagusha nilianguka chali hivyo niliweza kumuona sura na mwonekano wake, ni mrefu, maji ya kunde, mwili wake ni wa mazoezi, macho yake yametoka hivi, mrefu, si mweupe wala mweusi.
Wakili: Ulipofika Kituo cha Polisi, nini kiliendelea?
Shahidi: Nilitoa maelezo, nikapewa fomu namba tatu (PF3) nikapelekwa hospitali ya Amana.
Wakili: Fafanua Amana uliifahamu vipi wakati ulikuwa huoni?
Shahidi: Nilisikia sauti ya 'ambulance' (gari la wagonjwa) pamoja na milio ya vitanda na baadaye nikapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakili: Ulipata huduma gani Amana?
Shahidi: Waliniziba macho, waliniziba mgongoni na tumboni.
Wakili: Halafu baada ya kufika Muhimbili?
Shahidi: Nililetewa kitabu cha kusaini kwa maana wazazi wangu hawakuwapo na nilihitajika kufanyiwa operesheni. Baada ya muda, akaja daktari wa macho akahoji mbona huyu mtu macho yametolewa?
Wakili: Hospitali ulikaa muda gani?
Shahidi: Siku sita kwa mara ya kwanza.
Wakili: Kwa mara nyingine je?
Shahidi: Nilikaa siku moja asubuhi hadi jioni.
Wakili: Je, unaweza kuionyesha Mahakama sehemu uliyochomwa visu machoni?
Shahidi: Ndiyo
Shahidi huyo alivua miwani na kuonyesha macho yake yalivyoharibiwa na kuibua simanzi mahakamani hapo.
Wakili: Na mwilini hali ikoje?
Shahidi: Hali haikuwa nzuri kwa sababu nilichomwa visu vingi.
Wakili: Je, kwa sasa unaweza kuionyesha Mahakama majeraha ya mgongoni?
Shahidi: Ndiyo
Shahidi huyo alivua shati lake na kuonyesha sehemu za mwili wake uliojeruhiwa, hali iliyoonekana kuibua mshituko miongoni mwa watu waliohudhuriwa kusikilia kesi hiyo.
Wakili: Kitu chochote ambacho unataka kuieleza Mahakama?
Shahidi: Nina watoto wangu wanasoma na wanahitaji ada, nimepanga, ninahitaji kodi ya kulipa, na kwa sasa sina kazi nakaa nyumbani tu.
Baada ya Wakili Katuga kumaliza kumhoji shahidi huyo, Wakili wa Mshitakiwa, Nassoro, naye alimuuliza maswali kadhaa shahidi huyo kama ifuatavyo:
Wakili: Wazo la kwenda Buguruni Septemba 6 ulilipata ukiwa wapi?
Shahidi: Sikuwa na wazo la kwenda Buguruni.
Wakili: Wafanyabiashara Buguruni walikuwa wangapi?
Shahidi: Siwezi kukadiria
Wakili: Kuna maelezo kuwa wewe ni mwizi maeneo ya Buguruni, wewe unalisemaje?
Shahidi: Mimi siyo mwizi na Buguruni sikuwahi kufika na ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika eneo lile.
Wakili: Temeke unapajua?
Shahidi: Napajua, lakini sijawahi kufika.
Wakili: Tazara unapajua?
Shahidi: Napasikia, lakini sijawahi kufika.
Wakili: Maeneo ya Ilala Bungoni?
Shahidi: Ilala napajua, lakini sijawahi kushuka, navijua vituo vya daladala tu.
Wakili: Ndiyo maana tunasema wewe una historia ya wizi, lakini unaficha. Kituo cha Buguruni Polisi kipo umbali gani na sehemu ilipotokea tukio?
Shahidi: Sijui
Wakili: Kwa makadirio je?
Shahidi: Sijui
Wakili: Siku hiyo ya tukio wewe kama kawaida yako ulikuwa unakwenda Buguruni kununua simu na vifaa vya wizi na ndiyo maana watu hawakukusaidia, unasemaje?
Shahidi: Siyo kweli, sijawahi kununua vifaa vya simu ya mkononi wala kufanya biashara na vibaka.
Baada ya Wakili Nassoro kumaliza kumhoji, Wakili wa Serikali, Katuga naye akamhoji tena kama ifuatavyo:
Wakili: 'Statement' (taarifa) ya polisi uliwahi kusomewa?
Shahidi: Hapana
Wakili: Je, uliwahi kukamatwa na kufikishwa katika kituo chochote cha polisi?
Shahidi: Hapana
Wakili: Je, kununua vituu vya wizi?
Shahidi: Hapana
Wakili: Je, kuna uhalali wa kumpiga mtu na kumtoa macho hata kama ni mwizi?
Shahidi: Hakuna uhalali wowote.
Baada ya mahojiano hayo ya mawakili na shahidi, Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 28, mwaka huu wakati shahidi wa pili atakapotoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment