Image
Image

Waziri Mkuu aagiza viongozi idara ya uhamiaji kuandaa semina kwa wahudumu wa hoteli na Gesti.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kuandaa semina za mafunzo ya elimu ya uraia kwa wahudumu ya hoteli na nyumba za kulala wageni nchini ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Januari 19, 2017) mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Njombe na kupokea taarifa ya mkoa wa Njombe iliyotolewa na mkuu wa mkoa huo Bw. Christopher Ole Sendeka.
Katika taarifa hiyo Bw. Ole Sendeka alisema kwenye kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba, 2016 Idara ya Uhamiaji ilibaini kuwepo kwa raia 119 wa kigeni ndani ya mkoa huo, ambapo wahamiaji haramu 42 walikamatwa.
Waziri Mkuu alisema ni hatari kwa mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya raia wa kigeni walioingia nchini bila ya kufuata utaratibu hivyo aliitaka Idara hiyo ijipange vizuri ili kudhibiti watu wa aina hiyo.
“Anzisheni utaratibu wa kutoa semina kwa wahudumu wa hoteli na nyumba za kulala wageni. Hawa wakipata elimu ya uraia watawasaidia katika kutoa taarifa za kuwepo kwa wageni ambao wana mashaka na uraia wao,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa kujikita katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao.
Alisema lazima kuwe na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika halmashauri nchini. “fedha hizo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa yenye kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,”.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma kuibua maeneo mapya ya ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika katika utoaji wa huduma za jamii hivyo kuleta tija kwa Taifa.
Pia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na wasikubali kupokea miradi iliyojengwa chini ya kiwango.
Awali Mkuu wa mkoa huo alisema kati ya wahamiaji haramu 42 waliokamatwa 39 ni raia wa Ethiopia, wengine wanatoka Uganda (1), Burundi (1) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (1). Wote walifikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema Idara ya Uhamiaji inaendelea  na mikakati ya kuishirikisha jamii katika utoaji wa taarifa pindi wanapowatilia shaka kuhusu ukaazi wao ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na upanuzi wa huduma za uhamiaji.
Akizungumzia kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato mkuu wa mkoa alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 mkoa uliweza kukusanya kiasi cha sh. bilioni 7.07 sawa na asilimia 89.3 ya makisio ambayo yalikuwa sh. bilioni 7.92.
“Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 halmashauri zilikisia kukusanya kiasi cha sh. bilioni 8.22 ambapo katika kipindi cha nusu mwaka (Julai hadi Desemba, 2016) wameweza kukusanya jumla ya sh. bilioni 4.37 sawa na asilimia 53.2 ya makisio ya mwaka,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine maalumu za kielektroniki za kukusanyia mapato pamoja na kuondoa utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mawakala katika vyanzo vingi.
Aidha, Ole Sendeka alisema halmashauri za mkoa huo zinaendelea kupitia upya sheria ndogo za ukusanyaji wa mapato ili kuongeza vyanzo vya mapato pamoja na baadhi ya viwango vya kodi na tozo mbalimbali.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20, 2017.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment