Image
Image

Maofisa wa TRA kizimbani leo.

Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo la kukutwa akimiliki magari 19, mali isiyolingana na kipato chake halali.

Jennifer ameshtakiwa chini ya kifungu cha 27(1) (a) na (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Akisoma hati ya mashtaka hayo leo Jumanne, Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alidai kuwa mshtakiwa huyo kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA kama Ofisa Forodha Msaidizi alikutwa akimiliki magari 19.
Aliyataja magari hayo kuwa ni Toyota RAV4, Toyota RAV4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota Wish na Toyota Mark X.
Mengine ni Toyota Regiusage, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry yote yakiwa na thamani ya Sh 197,601,207 mali ambayo hailingani na kipato chake halali.
Wakili huyo alidai kuwa mshtakiwa huyo kati ya Machi 21 ,2012 na Machi 30, 2016 Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA kama ofisa forodha msaidizi alikutwa akiishi maisha ya kifahari yenye thamani ya Sh 333,255,556.24 fedha ambayo hailingani na kipato chake halali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Elisaria Mosha aliiomba Mahakama kumpatia dhamana mteja wake ya masharti nafuu.
Hakimu Shaidi, alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye atasaini bondi ya Sh 20 milioni.
Mshtakiwa huyo alikamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru.
Kesi imeahirishwa hadi Novemba 7, 2017 kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali (PH).
>>>http://www.mwananchi.co.tz/





Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment