Image
Image

Mawaziri Kairuki na Kigwangala wakutana kuweka mikakati ya ushindi katika wizara hizo.

MAWAZIRI wawili waliokabidhiwa wizara zinazotajwa kuwa ngumu kuziongoza, Angellah Kairuki wa Wizara ya Madini na Dk Hamisi Kigwangalla wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekutana na watendaji walio chini yao ili kuweka mikakati ya ushindi.
Waziri Kairuki alianza kujipanga kwa jana kukutana na watendaji wa wizara hiyo, taasisi na miradi inayosimamiwa na wizara hiyo ili kupata taarifa za kina kuhusu utendaji wao. Akizungumza, Waziri Kairuki alisema kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Madini za Dar es Salaam kilijadili mafanikio na changamoto za miradi ya maendeleo.
Watendaji ambao walikutana na Waziri Kairuki ni wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi asilia na Mafuta Tanzania (TEITI).
Kikao hicho pia kilishirikisha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. Naye Waziri Kigwangalla jana alikutana na kufanya mazungumzo na watumishi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara yake katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma.
Mbali ya kikao hicho nyeti kuhudhuriwa na Waziri Kigwangalla pia kiliwashirikisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu Aloyce Nzuki na Naibu Waziri Japhet Hasunga.
Kupitia kikao hicho, Waziri Kigwangalla aliwataka watumishi wote kuzingatia miiko ya kazi kwa kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake kama mtumishi aliyeaminiwa na Serikali. “Kwa pamoja tushirikiane kuijenga Wizara hii kama dhamana tuliyopewa na Rais wetu.
Sisi tumekuja hapa kusimamia yale yote ya dhana na malengo kusogeza mbele gurudumu la wizara hii. “Tunahitaji sana uzoefu wenu, ufanisi wenu kwani utaongeza kasi kwa kila mmoja wenu...aliyekuwa anakamata majangili watano, aongeze juhudi akamate majangili 10 ama zaidi.
Aliyekuwa analeta watalii wachache aongeze bidii alete wengi zaidi na wengine hivyo hivyo,” alisema. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Milanzi alimhakikishia Waziri Kigwangalla ushirikiano mkubwa katika kazi huku wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo na Wakuu wa Idara wa Wizara hiyo wakiwasilisha taarifa za namna ya kutekeleza majukumu yao.
Wizara za Maliasili na Utalii na iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini ambayo sasa imegawanywa na kuzaa wizara mbili, ndiyo wizara ambazo mawaziri wake wamekuwa wakiteuliwa na kukaa kwa muda mfupi kutokana na kuandamwa na kashifa mbalimbali.
Wakati rasilimali za madini zimekuwa chanzo kikuu cha mawaziri wa wizara hiyo kutumbuliwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za uingiaji wa mikataba yenye harufu ya rushwa, utoroshwaji wa wanyama na ujangili, zimekuwa ni sababu kubwa zinazowafanya mawaziri katika Wizara ya Malisili na Utalii kutumbuliwa mara kwa mara.
Waziri wa mwisho kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii alikuwa Profesa Jumanne Maghembe ambaye katika uteuzi wa Bazara jipya la Mawaziri lililotangazwa hivi karibuni na Rais John Magufuli hakuwepo huku Waziri wa mwisho kuiongoza Wizara ya Nishati na Madini alikuwa Profesa Sospeter Muhongo ambaye alitumbuliwa kutokana na kashfa ya utoroshwaji wa madini miezi michache iliyopita.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment