Image
Image

Serikali kudhibiti usalama wa meli na bahari

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu wakifuatilia majadiliano na kuchangia hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa  baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) kuwasilisha Muswada huo kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (aliyesimama) akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu baada ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Norman Sigalla King.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Saul H. Amon (aliyesimama) akichangia maoni yake kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa mbele ya Kamati hiyo baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) kuwasilisha Muswada huo kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma. 
Dododoma
............
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuanzisha chombo cha kuendesha na kudhibiti sekta ndogo ya usafiri majini, usalama wa meli na mazingira ya bahari ili kulinda maslahi mapana ya taifa. 
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu hoja ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupeleka Muswada Bungeni wa kutunga sheria ambayo itaanzisha Shirika  la Wakala wa Meli wa Taifa (NASAC)  ambao utasimamia usalama wa meli na bahari zetu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa bandari zetu kama mnavyojua bandarini kumekuwa na changamoto nyingi. “Hivi karibuni tumeshuhudia upotevu wa mali na vitu vingi pale bandarini kama vile madini na vitu vingine vinaingia bila utaratibu,” amefafanua Prof. Mbarawa. 
Ameongeza kuwa Serikali imeona ibadilishe mtazamo uliokuwepo zamani kupitia SUMATRA ambayo inasimamia masuala ya nchi kavu na majini, “Serikali imeona ianzishe chombo kingine ili kiweze kujikita kusamimia masuala ya usafiri wa majini pekee na masuala nyeti hasa ya uchumi wetu kama vile madini”. Chombo kimoja cha kutoa huduma na kudhibiti sio jambo geni. Hapa nchini tunayo taasisi ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) ambayo inatoa huduma ya anga na kudhibiti anga, hivyo Serikali inataka kufanya hivyo pia kwenye sekta ya usafiri wa majini. Hili si jambo geni kwa kuwa linafanyika kwenye nchi nyingine kama vile ya bandari ya Singapore na nchi nyingine ya India. 
Aidha, Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha chombo hiki. Pia amefafanua kuwa SUMATRA haitapokonywa majukumu yake bali nia ya Serikali ni kuitaka SUMATRA isimamie sekta ya nchi kavu tu kwa maana ya barabara, reli, magari ambayo ni sehemu kubwa na ina changamoto ambayo inahitajika kutatuliwa hivyo ijikite huko na sekta hii ndogo ya usafiri wa majini iwe na chombo kingine tofauti ili sheria iweze kutusaidia kukuza uchumi wa baharini na wa nchi kavu. 
Ni imani ya Serikali kuwa, kwa kuwa na chombo cha udhabiti cha sekta ya nchi kavu ambapo NASAC itaanzishwa kwa ajili ya sekta ya usafiri wa majini, utaziwezesha sekta hizi za majini na nchi kavu kukua vizuri hivyo kukuza uchumi wetu, watanzania watapata ajira na kampuni nyingi za meli zitaingia nchini na kufanya kazi kwa kuwa mahali ambapo hakuna udhibiti sekta haiwezi kukua, “angalieni sekta nyingine kama ya mawasiliano ambako kuna udhibiti mzuri na sekta inakua vizuri” amesema Prof. Mbarawa. Kwa mantiki hiyo, Serikali itawasilisha sheria ya SUMATRA Bungeni ili kufanyiwa maboresho ili iweze kuchangia vizuri ukuaji wa sekta ya nchi kavu na iende na wakati.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa azma ya Serikali ni nzuri katika muendelezo wa kuhakikisha kuwa taasisi zinazoanzishwa zina mgusa mlaji na kwa manufaa ya Serikali kwa ujumla. Serikali imejibu hoja zote za wadau na Kamati yetu inaendelea kuchambua hoja hizo ili kuhakikisha kuwa  inasimamia na kuishauri Serikali kwenye Muswada huu. Ni dhamira ya Kamati kuona kuwa biashara bandarini inaendelea kuimarishwa na kudhibitiwa; na nchi yetu sio pekee yenye bandari kwenye ukanda huu hivyo ni lengo la Kamati kuhakikisha kuwa Muswada huu unaopendekezwa unaboreshwa ili kuhakikisha una akisi ushindani. Ameongeza kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza udhibiti kwenye bandari yetu, hivyo huu ni mlolongo wa kusimamia na kudhibiti shughuli za uendeshaji wa bandari. 
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment