Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania limetakiwa kuharakisha kupeleka Muswada wa Sheria ya
Kusimamia Vyombo vya Habari bunge kusudi waandishi wa habari waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata kanuni na maadili ya taaluma ya Habari.
Kauli hiyo imetolewa na Baadhi ya wabunge wakati wakichangia
hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
nyakati tofauti, ambapo wabunge hao wameiipongeza wizara hiyo kwa kuridhia
Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari kwa kuwa itasaidia kukuza na kuiimarisha
taaluma ya habari hapa nchini tanzania.
Mbunge wa viti Maalum (CCM) Esther Bulaya alisema wakati umefika sasa kwa waandishi wa habari nchini kuandika habari
kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo ikiwa ni pamoja na kuandika habari
zilizofanyiwa utafiti wa kutosha na wakina
ili kutokuleta migogoro nchini.
Mhe. Bulaya amewataka waandishi wa habari wasitumie
vibaya uhuru wa habari walionao kwa
kutoa habari zinazoshabikia vyama vya siasa na zenye kuleta chuki na kupelekea
malumbano miongoni mwa chama au jamii moja na nyingine na badala yake waandike
habari zitakazo wafanya vijana waelewe nchi inakwenda wapi na sio habari
zitakazo wafanya vijana kujenga visasi.
Kwa upande wake mbunge wa Kondoa Kusini, Mhe. Juma Nkamia yeye
alisema kupatikana kwa sheria ya kusimamia vyombo vya habari kutasaidia
kuondokana na tatizo lililopo sasa la kuwa na waandishi wa habari wengi wasiokuwa
na sifa maarufu kama ‘makanjanja’.
Akizungumzia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Nkamia
aliitaka serikali kupitia wizara ya habari kuhakikisha inafanya kila
liwezekanalo kuyamalizia majengo yaliyopo Mikocheni ambayo yametelekezwa kwa
muda mrefu. Aliongeza kuwa majengo hayo yaliwekwa jiwe la msingi na Rais wa
awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi lakini mpaka sasa ni Serikali ya awamu ya
nne na majengo hayo hayajakamilika.
Mhe. Nkamia pia aliitaka serikali kuiongezea bajeti TBC
ili iweze kununua vifaa vipya na vya kisasa vya kurushia matangazo kwa kuwa
vifaa vilivyopo vimechakaa. Aliongeza kuwa matangazo ya TBC hivi sasa hukatika
katika kutokana na tatizo hilo.
Akiwasilisha hotuba ya Bajeti, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Dkt. Fenella Mukangara aliliambia bunge kuwa serikali imeridhia
kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya habari na muswada wa kutunga sheria
hiyo utawasilishwa bungeni hivi karibuni.


0 comments:
Post a Comment