Image
Image

EXCLUSIVE: FAHAMU KWA UCHACHE MAMBO YA MSINGI KUTOKA KWA MAREHEMU BOB MARLEY, NYOTA ILIYOKUWA NA MNG"AO WA KIPEKEE IKAFIFIKA GAFLA.

Kesho siku ya jumamosi ni siku ambayo Marasta wote duniani wanamkumbuka mwasisi na Mwanamuziki  ambaye alikuwa na kipaji cha pekee kwenye Muziki wa Reggae, nchini jamaika Bob Marley, nasiku hiyo kuwa Bob marley Day.
Napenda maendeleo ya muziki wetu, hicho ndicho kitu pekee ninachowaza. Nafikiria namna tunavyosonga mbele. Je, wajua? Muziki wetu unakua. Ndio maana kila siku watu wanakuja na nyimbo mpya, muziki utaendelea kusonga mbele daima.” Kauli ya marehemu Bob Marley Agosti, 1979.

Anatajwa kuwa mwasisi wa muziki wa reggae, mwanafalsafa na wakati mwingine nabii au mtabiri wa mambo mengi katika jamii.

Lakini si sifa hizo tu Bob Marley anabaki kuwa mwanamuziki aliyekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanyonge akitetea udhalimu duniani kote. Hakuwahi kubaki nyuma katika utetezi kwa wahitaji.


Kesho Bob anatimiza miaka 32  tangu afariki dunia mwaka 1981 kwa maradhi ya kansa,  Kwa hakika kuondoka kwake katika dunia hii kulileta simanzi kwa watu walioamini upendo huku wadhalimu wakifurahia kufariki kwake. 
Alifariki akiwaacha watoto 12, wane kati ya hao alizaa na mkewe Rita.

Hata hivyo, walioshangilia kifo cha mwanamuziki huyo ambaye kwa mtazamo mwingine waweza kumwita mwanaharakati walikuwa wamefanya kosa kubwa.

Ndiyo! Walifanya kosa kubwa sababu Bob Marley hakuondoka na sauti yake wala busara zake na wala hakuiacha dunia isiyo na fikra pevu. Sauti yake ingali ikinguruma hadi hii leo.

Na kama mara kadhaa alivyokuwa akipenda kusema kuwa sauti yake haitazimika na muziki wa reggae utadumu milele na milele.



 Hakika yametimia! Dunia bado inamkumbuka na wafuasi wa muziki huo wanaongezeka kwa maelfu katika kona nyingi duniani.

Alikuwa akiimba kwa kugusa kila kundi katika jamii, Alitangaza mapenzi kati ya mume na mke, akaimba juu ya mapenzi kwa watu wote, aliimba juu ya uhuru wa kutafakari na kuachana na dhuluma.

Kichwa chake kilijaa mambo mengi kwani hata lilipokuja suala la kisiasa na umoja wa kweli katika jamii, Bob aliyahubiri hayo yote katika tungo zake. Mfano ni katika vibao kama Africa Unite na Zimbabwe.

Alizaliwa akapewa jina la Robert Nesta Marley Februari 6, mwaka 1945 huko Saint Ann, Jamaica. Babaye alikuwa askari mwanamaji aliyeitwa Sinclair Marley, Huyu alikuwa raia wa Uingereza aliyekuja kuishi maisha ya ndoa na Cedelia Booker, Mjamaica Mweusi.

Baba wa Bob alifariki dunia wakati mwanamuziki huyo akiwa na umri wa miaka 10 ndipo mamaye akaamua wahamie Trenchtown Kingston.

Akiwa katika umri huo, Bob alijenga urafiki na Bunny Wailer na kwa pamoja wakajifunza muziki. Alipotimiza umri wa miaka 14, Bob aliachana na shule akajiingiza katika biashara ya kuchomelea vyuma.

Hata hivyo, katika muda wa ziada baada ya kazi alihakikisha anacheza reggae pamoja na Bunny Wailer na Joe Higgs.

Mwaka 1962 Bob Marley alifyatua single mbili lakini kwa bahati mbaya hazikuvuma kwa kipindi hicho, Mwaka mmoja baadaye wakaanzisha bendi yao pamoja na Bunny Wailer na Peter Tosh.

Awali bendi hiyo ikaitwa The Teenagers, Baadaye ikajulikana kama The Wailing Rudeboys, lakini ikabadilishwa tena kuitwa The Wailing Wailers,  Pia jina hili lilibadilishwa na kuwa The Wailers.


Hakuwa na mzaha kwani walipotoa baadhi ya nyimbo kama Simmer Down na Soul Rebel (1965) kundi hili liliteka masikio ya wengi. Mtunzi wa nyimbo hizo akiwa Marley.

Marley alijiingiza katika ndoa mwaka 1966 na kumwoa Rita Anderson, Aliishi miezi michache na mamaye mzazi huko Delaware.

Aliporejea Jamaica, Bob alianza kuwa na imani kali ya Urasta na hapo akaanza kuzisokota nywele zake kwa mtindo wa dreadlocks.

Albamu ya The Wailers ya mwaka 1974 Burnin' ikiwa na nyimbo kama vile I Shot The Sheriff na Get Up, Stand Up ziliwainua katika soko la kimataifa hasa katika bara la Ulaya na Marekani.

Kama ilivyosemwa na wahenga sana ivumayo sana haikawii kupasuka,  Ndivyo ilivyokuwa kwa kundi hilo kwani mwaka huo wa mafanikio wakaachana na kila mmoja kupiga muziki kivyake.

Pamoja na kuvunjika kwa kundi hilo, Bob Marley aliendelea kutumia jina la The Wailers na safari akaliita kundi lake Bob Marley & The Wailers.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kundi hilo kutengana wanamuziki hao walipiga muziki wa ska, Hii ni aina ya muziki ambao huchanganya vionjo vya muziki vya Caribbean, Calypso, American Jazz, rhythm na blues.

Alianza ziara katika maeneo mbalimbali na mwaka 1975 alipofyatua wimbo wa No Woman, No Cry, Bob akapata sifa nyingi kutokana na vionjo ndani ya wimbo huo na albamu yake ya Rastaman Vibration ikawa juu katika chati za Billboard.

Akaanza kuwa mwimbaji wa siasa na dini pia na alitumia kipindi hicho kuhubiri ambani na kujitambua katika utamaduni wao wa asili.

Jitihada zake hizo zikamweka katika wakati mgumu, alipata maadui wengi katika kipindi hicho na moja ya tukio moja baya ni kushambuliwa kwa risasi yeye, mkewe na meneja wake. Walinusurika.

Hata hivyo, hakurudi nyuma aliendelea kuwika akitangaza vita dhidi ya madhalimu na akawa balozi wa Jamaica na jamii ya Marasta kote duniani na kwa hakika kwa walio wengi walimfananisha na mungu mdogo.

Mwaka 1977, Bob Marley aligundua kidonda kwenye kidole chake,Aliamini kilitokana na mchezo wa mpira wa miguu lakini baadaye ikajulikana kuwa ni kansa.

Madaktari walimshauri wakiondoe kidole hicho lakini kwa imani yake ya dini Bob Marley alikataa, Matokeo yake ni kwamba kansa ikaenea mwilini.

Mwaka 1981 hali ya ugonjwa ilikuwa mbaya na alipokubali kupata tiba na alisema angependa afie nchini Jamaica lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo kwani ndege aliyokuwa akisafiria ilikwama Miami na huko yakamkuta mauti.

Bob Marley anatajwa katika sehemu mbalimbali duniani kuwa mtu aliyekuwa na kipawa cha mambo ya kiroho na mjuzi wa muziki wa reggae.

Mkewe Rita, watoto wake wa kiume Damian "Jr. Gong", Julian, Ziggy, Stephen, Ky-Mani na mabinti zake Cedelia na Sharon wanaendelea kumwenzi baba yao kwa kupiga reggae.

Amekufa akiacha nyuma tuzo nyingi za heshima huku nyimbo zake zikiwa zinaendelea kuvuma katika soko la duniani kote.

Wanazuoni na hata mashabiki wa nyimbo zake hupata mshangao kwamba ingekuwaje kama Bob Marley angekuwa hai hadi hii leo?

Wanajiuliza hilo kutokana na ukweli kwamba ubora wa kazi zake bado ni wa hali ya juu licha ya kuwa hayupo tena duniani.

Ameshapewa majina kama ‘Nyota wa kwanza katika dunia ya tatu’, ‘Nabii wa Rasta’, ‘Mwenye Maono’, na ‘Msanii Mwanamapinduzi’.

Alikuwa na karisma ya ajabu kutokana na uwezo wake wa kusema kitu na kikapokewa kwa kishindo na watu wengi huku kikiijenga jamii husika.

Bob alizikwa Alhamisi ya Mei 23, 1981, Alipewa heshima zote na watu wa Jamaica na maziko yalihudhuriwa na mafahari wawili Waziri Mkuu na kiongozi wa upinzani.,Aliyekufa akiwa na umri wa miaka 36.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment