Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba
waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya
zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi
mmoja.
Alisema
mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa
Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na
walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa
abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa yanayofanana si kitu cha kawaida
kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa forodha na vyombo vya usalama, sijui
walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji Mwakyembe.
Juzi
waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za
kulevya nchini, na alitekeleza ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari, kusema kuwa watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za
uwanja huo kudaka matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa
9:25 hadi saa 10:30 alfajiri.
Ameagiza
wafanyakazi hao wanne pamoja na askari polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba
mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa na wasichana wawili waliokamatwa Afrika
Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza)
kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa
waliokwenda na mzigo huo Afrika Kusini.
Mabegi
hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya ‘Crystal Methamphetamine’,
yalipitishwa na wasichana wawili wasanii aliowataja kuwa ni Agnes Gerald
‘Masogange’ na Melisa Edward ambao walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa
Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi
Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa
ni siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha
wiki mbili, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa
usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege
nchini.
Saa
nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa
kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34
ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango
ulivyosukwa
Alisema
siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa
uwanja huo akiwa anazungukazunguka eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana
ahadi na kukutana na mtu fulani.
“Kamera
pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya
jengo la abiria huku akizungumza na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa
kwa wafanyakazi wa eneo la ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati
huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha askari polisi anayetuhumiwa kuhusika
katika mpango huo akiwa anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama
vile anasubiri kitu fulani.” MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment