Image
Image

MWAKYEMBE AWALIPUA POLISI JUU YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.



Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amehoji kesi 36 zinazohusiana na dawa za kulevya ambazo Jeshi la Polisi limekaa kimya kwa kutoeleza hatua zilipofikia, hali ambayo inatia shaka na kudhoofisha vita dhidi ya biashara hiyo haramu.



Alisema hayo juzi wakati akihojiwa na televisheni ya Channel Ten kuhusu serikali imejipanga vipi kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya ambayo inaonekana kukithiri nchini na kuathiri asilimia kubwa ya vijana.



Dk. Mwakyembe alisema ili Watanzania wafahamu nini kinachoendelea kuhusiana na kesi hizo, ameahidi kuzifuatilia ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na biashara hiyo.



“Nitazifuatilia hizo kesi kwa kumshirikisha waziri mwenzangu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ili tujue hizo kesi zimefikia wapi na pia je, tule (ile) tumifuko (mifuko) twa (ya) dawa za kulevya zimewekwa wapi? Tusije tukakuta kuna mchanga ndani yake,” alisema Dk. Mwakyembe.



Kuhusu baadhi ya vigogo kudaiwa kujihusisha na biashara hiyo, alisema kama yupo mtu ambaye anawafahamu kwa majina vigogo hao ampelekee taarifa kwani suala hili lilipofikia sasa halihitaji usiri.



Dk. Mwakyembe alisema wizara yake itawasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili balozi za Tanzania zilizopo nje, zianze kubana watu wanaojihusisha na biashara hiyo.



Kuhusu maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), waliodaiwa kula njama za kusafirisha dawa za kulevya kilo 150 zilizokamatwa nchini Afrika Kusini, alisema atashangaa iwapo atasikia kuwa wamepeleleza na ushahidi haujajitosheleza.



Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja vya ndege ambavyo vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya nchini, hatua inayofuata ni kubaini wanaowatuma watu wanaokamatwa wakisafirisha dawa hizo.



Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja vya ndege ambavyo vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya hapa nchini, hatua inayofuata ni kufanya utafiti watu wanaokamatwa wakisafirisha dawa hizo ni nani anayewatuma.



Dk. Mwakyembe alisema biashara hiyo itaweza kukoma tu iwapo mipaka yote itadhibitiwa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.



Agosti 15 mwaka huu, Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa kwa dawa za kulevya kutaka wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya.



Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama hao watakaofukuzwa kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya kuwa ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.



Mbali na maofisa hao, pia aliliagiza Jeshi la Polisi kumwondoa mara moja katika uwanja huo, askari wake, Koplo Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya dawa za kulevya, yaliyokamatwa nchini Afrika Kusini.



Pia alisema polisi inapaswa kumsaka Nassoro Said Mangunga aliyevikwepa vyombo vya dola nchini Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo. 



Dk. Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Mohamed Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ili kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai.

Pia ameiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha kwa mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya na hivyo kuliletea Taifa fedheha kubwa.



Alisema ameamua kuchukua hatua hizo kwa kuwa tukio hilo siyo la kwanza, bali ni sehemu ya matukio mengi ya upitishaji wa dawa hizo katika uwanja wa JNIA, ambayo taarifa zake zinaifikia serikali pale watuhumiwa wanapokamatwa nje ya nchi wakitokea Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment