Image
Image

USHURU WA MALORI : YALIYO TOKEA MPAKANI RUSUMO YASIJIRUDIE.


Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mizigo Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay anasema Serikali imechukua uamuzi wa busara kushusha ushuru kwani malori ya Tanzania ni mengi kuliko ya Rwanda.
 
Kama hali ingebaki kama ilivyokuwa, msafirishaji angepandisha bei ya kusafirisha mzigo na kusababisha bidhaa kuuzwa kwa bei ya juu zaidi madukani.

Hali ya biashara kati ya Tanzania na Rwanda imekuwa katika hali ya wasiwasi tangu ilipoamua kupandisha ushuru mara tatu zaidi mpaka kufikia dola 500 za Marekani sawa na Sh800,000 kwa malori ya Tanzania.

Wasiwasi huo umesababisha Mawaziri wa Fedha wa nchi hizo kukutana kumaliza tatizo hilo kwa kurudisha viwango vya awali. Pamoja na kwamba ushuru umerejeshwa katika hali ya kawaida,  umesababisha malori takribani 300 kuwa katika hali ngumu mpakani mwa Tanzania na Rwanda katika eneo la Rusumo.

Awali ushuru huo ulikuwa Dola 152 za Marekani sawa na Sh243,200, lakini madereva wa Tanzania walipigwa butwaa ghafla walipotakiwa kulipa Dola 500 za Marekani sawa na Sh800,000 na kusababisha malori takribani 200 kukwama mpakani hapo kutokana na kushindwa  kulipa kiwango hicho.

Kutokana na malori hayo kuwa mengi foleni ilifikia kiasi cha kilometa 20 kutoka Rusumo mpaka Benaco.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk Charles Tizeba alilazimika kuzungumza na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba na walikubaliana kuongeza wiki moja ili malori hayo ya Tanzania yapite kwa kutumia ushuru wa zamani wakati yakisubiri ushuru mpya kuanza.
Tatoa wanasemaje?

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mizigo Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay anasema Serikali imechukua uamuzi wa busara kushusha ushuru kwani malori ya Tanzania ni mengi kuliko ya Rwanda.
Anasema Tanzania ina wastani wa malori 200 hadi 300 yanayofanya safari zake nchini Rwanda wakati Rwanda ina malori yasiyozidi 20 ambayo yanafanya safari zake Tanzania kwa hiyo Tanzania bado ina nafasi kubwa kibiashara.

Lukumay anasema makubaliano ambayo yamefikiwa kati ya nchi hizo, ni mwanzo mzuri kwa kuwa matatizo kama hayo yapo katika mpaka kati ya Tanzania na Zambia.

“Tusisubiri mambo yaharibike huku ndipo tuanze kuhangaika, yashughulikiwe sasa.
“Serikali ikae na wasafirishaji kwa ajili ya kutatua matatizo haya mapema na tuhakikishe hayajitokezi tena,”anatahadharisha Lukumay.

Lukumay anasema sekta ya usafirishaji inatoa ajira kwa watu zaidi ya milioni 1 nchini, na uzuri wake ni kwamba watu wengine tunaowapa ajira ni wale ambao hawana elimu kubwa.

Anasema kuna watu  wanaonufaika katika sekta ya usafirishaji kupitia sekta hiyo kwa mfano,  gereji na biashara za mama lishe ambazo hufanyika sehemu mbalimbali ambako malori yanasimama kwa muda.

Anaenda mbali zaidi na kubainisha kwamba katika Pato la Taifa (GDP), sekta ya usafirishaji imechangia kwa kiasi kikubwa kwani mwaka jana ilichangia asilimia 5.3 ya pato lote la taifa sawa na mwaka 2011.
Madereva wa Tanzania

Dereva wa malori, Iddi Mgaya akizungumza kutoka Goma nchini DRC anasema licha ya  gharama za ushuru  kushuka, lakini wanaona kama kuna kudorora kwa uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo tangu Tanzania ilipotangaza oparesheni ya kuondoa wahamiaji haramu mpakani mwa Mkoa wa Kagera na Rwanda. Jumla ya wahamiaji 6,000 walirejeshwa Rwanda hivi karibuni.

Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Anorld ambaye yupo Rusumo anasema hali ya mpakani hapo inawapa wakati mgumu kwani wamekuwa wakitaabika  na msongomano wa malori.

Anabainisha kwamba hivi sasa utaratibu wa kuvuka  mpakani umekuwa mrefu tofauti na siku zilizopita.
Anorld anasema hajaridhishwa na kitendo cha Tanzania kushusha ushuru kwani kuna tofauti kubwa ya umbali wa kilometa kutoka Dar es Salaam mpaka Rusumo na Rusumo hadi Kigali.

Dereva mwingine anayefanya safari kati ya nchi hizo mbili, Mwalimu Twaha anasema Serikali hizo kama zisingekubaliana kungetokea athari kubwa kiuchumi kwa madereva, wasafirishaji, wamiliki wa malori na wananchi wa nchi zote mbili.

“Kama hali ingebaki kama ilivyokuwa, msafirishaji angepandisha bei ya kusafirisha mzigo jambo ambalo lingesababaisha kuuzwa kwa bei ya juu zaidi madukani.

“Kazi zetu madereva zingepungua kwa sababu ya ukubwa wa gharama na sisi madereva tungekosa kazi,” anasema Twaha ambaye amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka 13 sasa,” anabainisha.

Twaha anaweka wazi kwamba wasafirishaji wengi wa mizigo wanapenda kwenda Rwanda kuliko nchi nyingine kwa sababu ni karibu (kuna umbali wa kilometa 1,460 kutoka Dar es Salaam hadi Kigali), lakini pia hakuna usumbufu.

“Rwanda ni njia ambayo siyo ngumu tofauti na nchi nyingine unaweza kwenda Rwanda hata mara nne ndani ya mwezi mmoja, ni rahisi unapofika ukishusha mzigo unaweza ukageuka na kurudi Dar es Salaam siku hiyohiyo,” anasema.
Chama cha wasafirishaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanexa, Mtemi Naluyaga anasema sakata la Rusumo limesababisha hasara kwa baadhi ya wasafirishaji wa bidhaa kutokana na malori mengi kukwama kwenye mpaka huo, kwani wafanyabiashara ni watu wanaopanga hesabu lini bidhaa zao zitafika mahali husika na kuuzwa.

Naluyaga anasema mpaka wa Rusumo siyo kwa ajili ya bidhaa zinazopelekwa Rwanda pekee bali hata nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
CHANZO: MWANANCHI
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

2 comments: