Image
Image

MAGUFULI: ACHARUKA ATOA MWEZI MMOJA KWA WATUMISHI WA SERIKALI WANAODAIWA MIKOPO YA NYUMBA MARA MOJA LA SIVYO WATAKIONA CHAMTEMA KUNI.


                                              Dk John Magufuli.
DAR ES SALAAM.
WAZIRI  wa Ujenzi, Dk John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa Serikali ambao wanadaiwa mikopo ya nyumba kulipa madeni yao mara moja na kuonya kwamba ikiwa watashindwa kulipa, watanyang’anywa nyumba hizo na watakopeshwa watu wengine.

Dk Magufuli ameibuka na hoja hiyo mpya, zikiwa ni siku chache tangu alipopigwa ‘stop’ na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutekeleza sheria ya kuondoa msamaha wa asilimia tano kwa mizigo inayozidi kwenye malori, hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa baina ya Serikali na wasafirishaji wa mizigo nchini.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za watumishi wa Serikali eneo la Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema watumishi 2500 hawajalipa mikopo ya nyumba walizonunua.

Dk Magufuli alionya kuwa atafuatilia suala hilo na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara moja, huku akimwomba Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kumuunga mkono kwenye jambo hilo, ambalo ni utekelezaji wa sheria za nchi.

“Naomba ifahamike kwamba tunapojenga nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma tunataka kuboresha makazi yao. Pia fedha tunazokusanya zinasaidia kujenga nyumba zaidi,” alisema Dk Magufuli. Hata hivyo alisema hadi sasa watumishi wa Serikali 4,900 ambao walikopa nyumba hizo tayari wamelipa madeni.

“Mimi nafanya kazi kwa kufuata sheria na kila mtumishi wa Serikali anafahamu jambo hilo, hivyo watu ambao wanajua tunawadai wakae kwa tahadhari, kwani ndani ya mwezi mmoja kama hawatalipa tutawachukulia hatua bila kupuuzia,” alionya Magufuli.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kutangaza kunyang’anya nyumba hizo, kwani alifanya hivyo mwishoni mwa Machi mwaka jana pale alipouagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba hizo kulipa madeni yao.

Dk Magufuli aliwataka TBA kutoa ilani ya maandishi inayowataka wahusika walipe fedha hizo ndani ya wiki moja vinginevyo wangenyang’anywa kwa maelezo kwamba wanachelewesha malengo ya TBA kujenga nyumba zaidi. 

Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizowahi kutolewa kuhusu kutekelezwa kwa amri hiyo iliyotolewa zaidi ya miezi 18 iliyopita.

Jana, Makamu wa Rais, Dk Bilal alimuunga mkono Magufuli akisema: “Naunga mkono tamko la Waziri wa Ujenzi kwamba ni lazima watumishi wa Serikali ambao wanakopeshwa nyumba walipe haraka ili fedha hizo zisaidie kujenga nyumba nyingine.”

Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika shughuli ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo la Bunju ‘B’ Kinondoni, Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, alisema ujenzi huo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iligharimu Sh2 bilioni na awamu ya pili Sh1 bilioni.

“Nyumba 851 zinazojengwa Bunju B ni sehemu ya ujenzi wa nyumba 4,400 katika Mkoa wa Dar es Salaam na nyumba 10,000 kwa nchi nzima,” alisema Mwakalinga.

Hafla hiyo ilisimama takriban kwa dakika 10 wakati Dk Bilal akitaka kuhutubia baada ya jenereta kushindwa kufanya kazi, hivyo kumlazimu kurudi kuketi kwenye kiti hadi umeme uliporejea. 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alilazimika kwenda kufuatilia suala hilo na mafundi waliokuwapo walifanikiwa kuunganisha mashine za kipaza sauti na umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hivyo Makamu wa Rais aliendelea kuhutubia. MWANANCHI
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment