Image
Image

Sekondari Dar yageuza wikiendi siku za masomo

WANAFUNZI wa Shule ya Seminari ya Kiislamu ya Mivumoni jijini Dar es Salaam, husoma kwa siku tano kama kawaida, lakini `wikiendi’ yao huwa siku za Alhamisi na Ijumaa. Hii ina maana kuwa siku za masomo huanza Jumamosi na kuendelea Jumapili, Jumatatu hadi Jumatano.

Kwa kawaida, siku za masomo wakati ambapo shule zinakuwa hazijafungwa huwa Jumatatu hadi Ijumaa, isipokuwa kwa siku za sikukuu za kitaifa.

Shule hiyo ya kutwa iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni eneo la Kinondoni B, iko chini ya msikiti wa Mtambani, ina wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne.

Hata hivyo, shule hiyo imetakiwa kubadili utaratibu wake wa siku za masomo, kwa maelezo kuwa unakwenda kinyume na taratibu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Imeelezwa kuwa utaratibu huo ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kanuni za nchi, kwani kwa kufanya hivyo shule hiyo inawakosesha watoto haki yao ya msingi.

Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda ya Dar es Salaam, Suzan Samuel alisema shule hiyo tayari imeshauriwa mara mbili, kubadili utaratibu huo ili kuendana na sheria zilizopangwa.

Alisema shule zote husajiliwa na Wizara ya Elimu, hivyo kutakiwa kufuata taratibu zilizopangwa na wizara hiyo, ikiwemo ya kufanya kazi kati ya Jumatatu mpaka Ijumaa, na si vinginevyo.

"Tulipata taarifa kuwa wana utaratibu huo, wakaguzi walikwenda kutembelea mara ya kwanza, kweli tukakuta watoto hawasomi Alhamisi na Ijumaa, tukawashauri lakini bado wanaendelea," alisema.

Alisisitiza kuwa ni kosa kubwa kwa wanafunzi kutosoma katika siku ya Alhamisi na Ijumaa.

"Kusoma Jumamosi na Jumapili hiyo ni juu yao, lakini kosa kubwa ni kutosoma siku hizo mbili za kazi, ambazo sheria yetu inasema hivyo," alisema.

Alisema tayari wamewapelekea barua ya kujieleza, kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka sheria zilizopo, lakini bado hawajajibu. Alisema pia barua nyingine wamepeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kwa kuwa na yeye ndiye mtendaji mkuu.

"Taratibu ziko wazi na zinajulikana kuwa shule zote zifuate sheria zilizopo, hata kama ni shule za seminari. Nadhani hata walipokwenda kuomba usajili wizarani, walikiri kufuata sheria, lakini sasa wamebadilika," alisema.

Alisema kama wangekuwa wamepata kibali kutoka wizarani, ingekuwa haina tatizo, lakini wao wameamua kufanya kienyeji.

Alisema kama kuna shule nyingine, zimejiamulia utaratibu wao, zihakikishe zinafuata sheria za nchi. Mkuu wa Shule hiyo, Dadi Hemed, akizungumza na gazeti hili, alisema hawaoni tatizo kwa wao kupumzika Alhamisi na Ijumaa, bali kitu cha muhimu ni kusoma siku tano, jambo ambalo wanalifanya.

Aliliambia gazeti hili kuwa wameamua kupumzika siku hizo mbili, kwa madai ya wanafunzi wa kidato cha pili na nne hufanya mitihani ya majaribio ya ndani ya shule.

"Kikubwa tunasoma siku tano kama shule zingine, tofauti ni hiyo ndogo tu, lakini hatuoni kama tuna tatizo kupumzika siku hizo na kusoma Jumamosi na Jumapili," alisema Hemed.

Hemed alikiri kupokea barua ya kutaka wajieleze, lakini alisema kuwa bado wanaifanyia kazi. Alisisitiza kuwa hakuna tatizo kupumzika siku hizo mbili.

Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa kwa masharti ya kutotajwa majina gazetini, walikuwa na maoni tofauti.

Mmoja wao anayesoma kidato cha pili, alisema utaratibu huo hauko sawa ila kwa kuwa ni maamuzi yamepitishwa haina jinsi inabidi wakubaliane nao. 

Alisema kimsingi inatakiwa waendane na shule zingine, lakini wanashangaa wao kupumzika siku hizo mbili.

“Wakati mwingine inatia uvivu kwenda shule, unaamka Jumapili asubuhi wenzako wamelala wewe inatakiwa kwenda shule. Inaweza ikachangia utoro kwa wanafunzi. 

Mwanafunzi mwingine anayesoma kidato cha nne, alisema kwa sasa utaratibu huo wanauona ni wa kawaida, lakini unawapa taabu wageni wanaoanza shule hiyo au kuhamia.



Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment