Image
Image

Muhongo aachia ngazi kwa shinikizo la kashfa ya Escrow iliyokuwa ikimwandama


Baada ya kusuasua kwa miezi kadhaa, hatimaye Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesalimu amri na kujiuzulu.
Nafasi yake  kuchukuliwa na  George Simbachawene, aliyewahi kuwa naibu wake. Uteuzi wa Simbachawene ulifanyika saa chache baada ya  Profesa huyo kuanchia ngazi.
Profesa Muhongo aliyedaiwa kuwa ni dalali wa kufanikisha uchotwaji wa Shilingi bilioni 300 kutoka kwenye akaunti ya Escrow iliyokuwa imefunguliwa na Tanesco na kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL, alisema anaondoka ili taifa lifanye shughuli za maendeleo badala ya kuendeleza mjadala wa Escrow.
Hatua ya kujiuzulu aliitangaza jana jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari na kusisitiza kuwa lazima serikali ifike mahali ifanye kazi na kuwakwamua wananchi kwenye umaskini badala ya kujadili jambo moja.
“Baada ya kutafakari na kukubaliana na wakubwa wa juu, naona lazima maslahi ya taifa yapewe kipaumbele kuliko cheo cha mtu mmoja.”
“Ndugu zangu waliopo vijijini wanataka umaskini uwatoke, hivyo viwanda vinataka umeme ili vijiendeshe, vijana wanataka elimu, sidhani cheo changu ni muhimu kuliko hawa wanaoteseka,” alisema na kuongeza:
Pia alisema anaondoka ili kuiwezesha CCM kutumia vikao vyake kujadili jinsi ya kuwatumikia Watanzania badala ya kugeuka kuwa uwanja wa Escrow.
“Nilazima ifike mwisho sasa, Bunge lijadili mambo mengine ya maendeleo badala ya kutumia fedha za wanyonge wanaolipa kodi kujadili suala moja tu,”alisema.
Profesa Muhongo alisema Bunge lililopita alizungumzia vizuri kuhusu sakata hilo na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) iliongea kwa upande wake na mwisho maazimio yalifikiwa na kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema baada ya maazimio hayo kukabidhiwa kwa Rais alifafanua kwa undani na kwa urefu ambapo maelezo aliyotoa hayakupishana na yake.
“Lakini bado naona mjadala haufiki mwisho, ni lazima kila kitu kiwe na tamati nadhani mimi ni suluhisho la hili, ndani ya Escrow kuna mivutano ya kisiasa isiyokuwa na mwisho,” alisema na kuongeza:
“Ipo mivutano ya kibiashara ambapo Watanzania, serikali, CCM  na mimi pia tumechoka kuisikiliza ,” alisema.
Aliongeza:“Kuna wivu, chuki na fitina kama kweli dira yetu ya maendeleo tunataka taifa liondokane na umaskini ifikapo mwaka 2025 lazima tufike mwisho sasa badala ya kuendeleza chuki, wivu, ubinafsi, mivutano ya kibiashara na kisiasa, tujadili maendeleo,”alisema.
Hata hivyo kujiuzulu huko kunakuja muda mfupi kwani hivi karibuni Muhongo alikuwa katika ziara za mikoa ya Mara na Simiyu ambapo katika mikutano yake ambayo alitoa kipaza sauti kwa wananchi kumuuliza maswali, hakuna sehemu ambako watu walizungumzia sakata la Escrow.
“Vijijini wanataka maendeleo hawajui Escrow kwa sababu haiwapatii huduma za kijamii kama maji na umeme, tufike mahali tushughulikie mambo ya maendeleo sasa,” alisema na kuongeza:
 “Nimemuomba Rais niachane na nafasi ya uwaziri hakuna sababu ya kulumbana tunapoteza nguvu na rasilimali zetu,” alisema.
SABABU ZA KUJIUZULU
Profesa Muhongo alisema ili serikali ishughulikie matatizo ya wananchi badala ya Escrow, ili chama chake cha CCM, kitatue kero za wananchi, akirejea bungeni awe mtu wakawaida na kutoa fursa ya mijadala mingine badala ya Escrow.
Nyingine ni Watanzania wamechoka na Escrow haina tija kuijadili asubuhi hadi jioni wapate fursa ya kuongea mambo ya maendeleo kuliko malumbano, ana familia kwa hiyo haiwezi kuamka kila siku na kusikiliza Escrow na mwisho ni sakata la Escrow kuwa na mivutano ya uongozi na madaraka.
MUHONGO DALALI WA IPTL
Kujiuzulu kwa Muhongo kutakuwa na mwangwi huu wa maelezo ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe aliyoyatoa bungeni Novemba mwaka jana wakati wa kujadili sakata la Escrow:
Kamati imethibitisha kuwa Profesa Muhongo, alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Singh Sethi mmiliki wa kampuni ya PAP iliyoinunua IPTL na mwekezaji mwenza wa IPTL James Rugemalira tena katika ofisi ya umma yaani ndani ya Wizara ya Nishati na Madini.
Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL.
Iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, ongezeko la mtaji, ushuru wa stempu ambazo ni takribani Shilingi bilioni 30.
Kwa hiyo Kamati ikapendekeza kwa Rais kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana sababu kadhaa zikiwamo udalali.
SHINIKIZO LA KIMATAIFA
Desemba mwaka jana Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti kuwa Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni 700 sawa na Shilingi trilioni 1.1 zilizokuwa zitolewe na mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) la Marekani kutokana na ufisadi na ruswa ya kutisha inayotikisa nchi.
Shinikizo hilo la wahisani lilikuja wakati Rais anasubiriwa kutoa maamuzi magumu na kutekeleza mapendekezo ya Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow ambayo Muhongo anadaiwa kuwa dalali.
Ubalozi wa Marekani ulieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba mwaka jana wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini.
Hilo pia ni wimbi lililoitikisa serikali na kusababisha Muhongo ang’oke.

WIMBI LA KUJIUZULU
Profesa Muhongo anakuwa waziri wa nne wa Nishati na Madini anayejiuzulu kwenye serikali ya Rais Kikwete.
Wa kwanza alikuwa Nazir Karamagi aliyeachia ngazi mwaka 2008 baada ya kuhusishwa na hizaya (kashfa) ya Richmond. Pamoja naye Naibu Waziri Profesa Ibrahim Msabaha naye aliondoka.
Mwaka 2012 Waziri William Ngeleja aliyechukua nafasi ya Karamagi, aliondolewa kwenye baraza la mawaziri kwa kushindwa kutimiza majukumu yake akionekana kuwa waziri mzigo.
Safari hii wimbi la kujiuzulu limemuondoa Profesa Muhongo aliyeteuliwa mwaka 2012 kuwa mbunge na waziri.


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment