Image
Image

Taasisi ya Hakielimu yaukosoa mpango wa matokeo makubwa BRN


 Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mkutano huo uliofanyika katika ofisi za HakiElimu leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Wengine kushoto na kulia ni maofisa wa taasisi ya HakiElimu wakiwa katika mkutano huo.
                                                                       Na Joachim Mushi
TAASISI ya HakiElimu imeukosoa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ‘Big Results Now’ (BRN) unaotekelezwa na Serikali katika sekta nyeti ikiwemo elimu kwa madai kuwa matokeo yake kwenye sekta ya elimu sio ya kuridhisha.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya tathmini ya kitaalamu iliofanywa katika utekelezaji wa BRN kweye sekta ya elimu.
Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha ya ufaulu huu kuonekana kupanda ghafla kuna changamoto nyingi katika sekta ya elimu ambazo bado hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
“…Mfano migogoro ya mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama za utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi. Mpango wa BRN ni mzuri lakini muda uliowekwa kutekeleza malengo yake ni mfupi kwa kuzingatia mazingira ya utoaji elimu na changamoto zake,” alisema Boniventura.
Kaimu huyo Mkurugenzi alibainisha kuwa kumekuwepo na mabadiliko ya mara kwa mara katika sekta ya elimu likiwemo la hivi karibuni la alama za ufaulu na mabadiliko ya viwango vya upimaji wa matokeo ya wanafunzi ambayo yameleta mabadiliko katika takwimu za ufaulu lakini yasitumike kama ishara ya kuimarika kwa ubora wa elimu itolewayo.
Aidha aliongeza kuwa matokeo mazuri yoyote ya mipango ya maendeleo ikiwemo elimu yanahitaji uwekezaji wa kutosha, ilhali shule za msingi na sekondari zina changamoto nyingi za upungufu wa miundombinu jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kiufasaha zaidi tofauti na inavyofanyika sasa.
“…Serikali haina budi kutafakari na kuona kama uwekezaji uliofanyika mpaka sasa umefanyika kiasi cha kutosha kuleta matokeo kusudiwa. Hali ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu si nzuri ambapo asilimia 24 tu ya fedha ya bajeti inapangwa kwenye miradi ya maendeleo inayohusu miundominu ilihali matumizi ya kawaida yakiwa asilimia 74 ya bajeti ya elimu,” alisema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment