Image
Image

Jeshi la kujenga taifa JKT latoa tamko zito kwa vijana walio maliza mafunzo yake nakutangaza kuandamana ili kudai ajira


JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana waliohitimu mafunzo ndani ya jeshi hilo ambao wanataka kuandamana kwenda Ikulu kwa ajili ya kushinikiza kupata ajira, watambue kuwa walikula kiapo cha utii, wakati wa kuhitimu mafunzo ya JKT, hivyo suala la kuandamana ni kinyume cha kiapo chao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana Dar es Salaam na Ofisa habari wa JKT, Meja Emmanuel Muruga, vijana hao wanatakiwa kutambua kuwa tatizo la ajira si kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima na Tanzania ikiwemo.
JKT limewataka vijana hao kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe. Alisema kuwa vijana hao walitumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza mkataba wa miaka miwili, hivyo shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na viongozi wengine mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza kuwa, JKT halitoi ajira," alisisitiza Meja Muruga.
Meja Muruga alisema hivi karibuni wakati nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa urais na wabunge mwaka huu, kumezuka mtindo wa makundi ya vijana waliopitia JKT katika Operesheni mbalimbali kuomba kuandamana kwenda Ikulu kudai ajira.
"Madai hayo yanayopingana na dhana ya JKT na kauli ya Rais kuwa Jeshi la Kujenga Taifa haliajiri, bali vijana hujiunga kwa hiari kwa kujitolea na baada ya mkataba wa miaka miwili wanatakiwa kurejea walikotoka," alisisitiza.
Alisema kuwa Rais Kikwete, amewahi kutoa agizo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, taasisi za Serikali na kuziomba zile zisizo za kiserikali kutoa ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT kulingana na sifa za kijana na nafasi zilizopo.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi mwaka jana, jumla ya vijana 104,594 wamejiunga na JKT wakiwemo wavulana 76,832 na wasichana 27,762.
Meja Muruga alisema katika kipindi hicho, jumla ya operesheni 13 katika mafunzo ya JKT zimefanyika, Operesheni hizo ni pamoja na Operesheni Mkapa mwaka 2001,miaka 40 ya JKT mwaka 2002, utandawazi mwaka 2004 na Operesheni Jiajiri mwaka 2005.
Alisema zingine ni pamoja na Kasi Mpya mwaka 2006, Maisha Bora mwaka 2007, Uadilifu mwaka 2008, Kilimo Kwanza mwaka 2009 na Operesheni Uzalendo mwaka (2010), Miaka 50 ya Uhuru (2011), Sensa mwaka 2012, Miaka 50 ya JKT (2013) na Miaka 50 ya Muungano (2014).
Alisema JKT lilianzishwa Julai 10, 1963 na serikali kwa lengo la kuwaweka pamoja vijana wa nchi hii na kuwapa malezi kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za matabaka zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.
Alitaja baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa JKT kuwa ni,Kubadili fikra za vijana wa nchi hii kutoka ile hali ya ukoloni kutegemea nchi nyingine kuleta maendeleo,kukusanya nguvu za vijana wote wa nchi hii na kuzielekeza kwa umoja wao kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya taifa.
Alisema pia ni kuwafunza vijana kujenga mshikamano na moja wa kitaifa, ili kulinda uhuru wa Taifa lao na pia JKT linaunganisha vijana bila kujali itikadi zao, dini, elimu, jinsia na mali ili kuwalea kuwa wazalendo kwa taifa lao na kupenda kuitumikia nchi yao.
Alisema kuwa pamoja na dhana ya kufunzwa uzalendo, pia stadi mbalimbali za kazi hufundishwa kwa vijana hao ili waweze kujiajiri, pindi wamalizapo mikataba yao ya kujitolea ya miaka miwili.
Meja huyo alisema Serikali ilirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001, baada ya kusitishwa mwaka 1994.
Alisema kuwa masharti ya kujiunga na JKT kwa vijana wa kujitolea kabla ya kujiunga na JKT hutakiwa kuyajua masharti na kuzifahamu taratibu za kujiunga na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira.
Alifafanua kuwa moja ya kipengele cha kujiunga na JKT kinaeleza kuwa; "Kwa kipindi chote nitakachokuwa ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie ajira/kazi."
Alisema kuwa kipengele hiki kinaainisha masharti ya makubaliano kati ya Jeshi la Kujenga Taifa na kijana kabla ya kujiunga na kupatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.
Alisema kuwa, tangu mwaka 2003 hadi 2014 jumla ya vijana 24,708 wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670 wameajiriwa na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Jeshi la Polisi vijana 3,965 wavulana wakiwa 2,943 na wasichana 1,022, Magereza vijana 2,139 wavulana 2,044 na wasichana ni 95, Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa ni 78 na wasichana ni 22 na taasisi zingine vijana 592.
Alisema kuwa Vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama TANAPA, Geita Gold Mine, Bandari na African Gold Mine.
"Kwa maelezo ya hapo juu utaona kuwa Jeshi la Kujenga Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za serikari na binafsi," alisema.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment