Image
Image

Warioba avitaka vyama vya siasa kuzingatia matakwa ya wananchi katika kura ya maoni kwenye katiba pendekezwa

WAZIRI Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba amevitaka vyama vya siasa kuzingatia matakwa ya wananchi katika suala zima la Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na badala ya kuwagawa.
Aidha, Warioba amesema anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa katika Rasimu ya Katiba, ipo siku vitafanyiwa kazi kuondoa migongano huku akisisitiza, kisheria kura ya maoni siyo mwisho wa mchakato.
Warioba alisema kwa sasa, badala ya kuwaweka wananchi pamoja na kukubaliana wanachotaka , upo mvutano huku wengine wakitaka Katiba Iliyopendekezwa ikubaliwe na wengine wakitaka wananchi waikatae.
“Kwa suala hili la kundi la Ukawa kuwasihi wafuasi wake kutoshiriki katika upigaji kura ya maoni, inaonyesha dhahiri hakuna maridhiano na wananchi kwani badala ya kujua matakwa yao, vyama vya siasa vinawagawa wananchi katika suala hilo jambo ambalo linaonyesha vyama hivyo vinajitazama vyenyewe,” alisema.
Alikuwa akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV. Alisema suala la kupiga kura ya maoni ni kuangalia maridhiano na wananchi na si vyama vya siasa.
Alisema hata katika mchakato wa awali, waliangalia maridhiano ya wananchi na walihakikisha maoni yao yanaingia kwenye Katiba pendekezwa.
Alisema vyama vya siasa vinataka maridhiano yao bila kuangalia matakwa ya wananchi na kukubaliana jambo, alilosema ni tatizo.
Muungano, madaraka Alisisitiza kwamba anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa, ipo siku vitafanyiwa kazi kuondoa migongano.
Alisema katika Katiba Inayopendekezwa, suala la mgawanyo wa madaraka halijaainishwa lakini anavyoona maendeleo katika dunia na matatizo, ipo siku lazima madaraka yatenganishwe, kwani kutakuwa na migongano kati ya Serikali na Bunge.
Alisema ingawa masuala hayo hayajaingizwa katika Katiba Inayopendekezwa, kama ilivyokuwa kwenye rasimu iliyoandaliwa na Tume aliyokuwa akiiongoza, anaamini kutakuwa na mabadiliko kabla ya kura ya maoni au baada kwa kuwa hayaepukiki.
“Matatizo haya ya wazi ya masuala kama ya mgongano wa madaraka na Muungano yatafanywa kabla au baada ya kura ya maoni kwani kuna mambo katika Katiba pendekezwa hayawezi kutekelezwa na hayazungumziki,” alisema.
Maadili Akizungumzia suala la maadili,Warioba alisema sheria ya maadili ipo, lakini haina nguvu kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine.
Alitoa mfano wa Ufilipino akisema walikuwa na sheria hiyo lakini wakaweka kwenye katiba iwe rahisi kutekelezwa. Alitaja pia Namibia na Kenya.
Alisema suala la mgawanyo wa madaraka bado ni muhimu kwani kwa kutenganisha, kunaweza kusaidia katika uwajibikaji . Alitoa mfano wa sakata la Tegeta Escrow bungeni na kusema Bunge na Serikali ziliingiliana madaraka badala ya serikali kuwa na kauli moja.
“Hebu angalia suala la Bunge kumfukuza Katibu Mkuu, hii siyo kazi yake, lilichanganya madaraka, kama Bunge haliridhiki na mwenendo wa serikali haliwezi kwenda kufukuza watumishi wa serikali.
Bunge linatakiwa kusema kutokuwa na imani na serikali na siyo kufurahia kusema fulani afukuzwe. Siyo utaratibu mzuri,” alisema.
Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema kazi ya Bunge ni kusimamia serikali na siyo kufukuza watu, kwani wakati mwingine kunakuwa na suala la visasi na kufukuza watumishi ambao hawahusiki.
Serikali mbili Kuhusu Muungano, alisema, “Hili jambo ni ‘serious’(nyeti) lazima kufika wakati kuwa na nchi moja na hata kuangalia jinsi ya kuweka sawa suala la muundo wa serikali.”
Alisisitiza msimamo wake kwamba yeye ni muumini wa Muundo wa serikali mbili kwenda moja na siyo muumini wa serikali tatu. Alipendekeza kwenda hatua kwa hatua hata baada ya miaka 100 kupata serikali moja.
Kura ya maoni Warioba alisema siku ya kupiga kura ya maoni, inaweza kubadilishwa kwani haiko kisheria na haitaathiri mchakato wa kupata Katiba mpya.
Alisema tarehe ya kupiga kura, imewekwa na wanaohusika na inaweza kuahirishwa kwa kadri wanavyoona maandalizi yamekamilika katika kuandikishwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment