Image
Image

BAJETI: Wabunge wamshukia Nyalandu.


Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Kambi ya Upinzani Bungeni jana waliungana kumbana Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wakisema amelikosesha Taifa mabilioni ya shilingi.
Hotuba zote mbili, ya kamati na upinzani, zilieleza kushangazwa na kitendo cha waziri huyo kupinga watalii kulipa tozo mara moja kila wanapoingia katika Hifadhi ya Serengeti na Ziwa Manyara, badala yake kung’ang’ania walipe mara mbili, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Bunge.
Akisoma taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli alisema, “Takwimu zinaonyesha kwamba tangu Julai 2014 hadi Machi 2015, hifadhi hizo mbili zilipoteza Sh1.4 bilioni kutokana na wizara kulazimisha tozo mara mbili. Kamati inahoji, kuna masilahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea Serikali mapato?”
Alisema licha ya Bunge kuazimia Nyalandu atekeleze hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomtaka kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli ndani ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hakuzingatia suala hilo.
“Kutokana na kuchelewa kuanza kutumika kwa tozo mpya kama ilivyoamriwa na Mahakama, Serikali imepoteza Sh3 bilioni hadi kufikia Machi 15, 2015. Kamati inamtaka waziri (Nyalandu) kulieleza Bunge nini kilimfanya akaidi kutekeleza hukumu iliyokuwa na masilahi kwa Taifa,” alisema Lembeli.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Fedha hizi Sh3 bilioni zingeweza kununulia madawati ya watoto wanaokaa chini, kununua vitanda vya wajawazito au kupunguza deni la (MSD) Bohari Kuu ya Dawa.”
Mchungaji Msigwa alisema ni aibu kwa Nyalandu ambaye ametangaza nia ya kugombea urais, kusimama na kusoma mafanikio ya wizara yake wakati amelisababishia Taifa hasara.
Katika hotuba yake, Msigwa pia aligusia ujangili wa wanyamapori na kuhoji sababu za Serikali kushikwa na kigugumizi cha kuteketeza tani 90 za shehena ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika maghala baada ya kukamatwa kutoka kwa watu mbalimbali.
Msigwa pia aliibua sakata la kusafirishwa kwa wanyama hai kwenda Uarabuni akiitaka Serikali iweke hadharani majina ya watu waliohusika.
Mbunge huyo wa Iringa Mjini alisema ni wakati sasa kwa Serikali kuanika uozo huo hadharani kwa kuwa suala la kusafirishwa kwa wanyama haliko mahakamani tena kama ambavyo Serikali imekuwa ikijificha humo.
“Tunaomba majibu sasa, nani alibeba wanyama wale maana kesi haiko tena mahakamani kama ambavyo mmekuwa mkitueleza,” alisema Msigwa.
Alisema Watanzania wamechoka kudanganywa kwa maneno matamu ya kuwapumbaza, wanachotaka ni kujua jinsi rasilimali zao zinavyotumiwa vibaya.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment