Image
Image

Siku tatu za kishindo; watano kutangaza nia CCM.


Ni siku tatu za hekaheka na kujenga hoja za kujinadi kuanzia kesho wakati makada wa CCM watakapotangaza kwenye mikutano ya hadhara sababu zilizowasukumu kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CCM ipo kwenye wakati mgumu wa kutafuta mrithi wa Jakaya Kikwete katika nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe nchini baada ya Rais huyo wa sasa kuongoza nchi kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu kutokana na utashi wa kikatiba.
Kutokana na hilo, zaidi ya makada 20 wanatajwa kuwa na nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais ili kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na watatakiwa kutangaza, kuchukua fomu na kuzirudisha ndani ya takribani siku 32 kabla ya Julai 2 ambayo ni siku ya mwisho iliyowekwa na chama hicho.
Wakati makada hao wa CCM wakijipanga kufanya shughuli kubwa za kutangaza nia ya kuomba wanachama wao wawape ridhaa ya kugombea urais, baadhi ya vyama vya upinzani vimeshatangaza ratiba zao lakini kinyang’anyiro kikubwa kitakuwa wakati vyama vilivyo chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapofanya mchujo wa kumpata mgombea atakayewakilisha umoja huo.
Kwa mujibu wa ratiba za makada wa CCM, kesho Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atafanya mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kutangaza rasmi nia ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.
Timu ya Lowassa, ambaye aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari mwanzoni mwa wiki kuwa atatangaza nia Mei 30, imekuwa ikitoa matangazo mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutaarifu tukio hilo la kuanza rasmi kwa safari aliyoiita “ya matumaini”.
Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mapema wiki hii, Lowassa alihifadhi majibu ya baadhi ya maswali, akisema ni sehemu ya masuala atakayozungumzia kwenye hotuba yake ya kutangaza dhamira yake ya kuomba urais.
Tukio hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha litarushwa moja kwa moja na vyombo vinane vya habari kwa muda wa saa nne kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 11:00 jioni.
Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa kumekuwa na maandalizi ya hali ya juu jijini Arusha kuelekea siku ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa watu mbalimbali wanaomuunga mkono wakiwamo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli, alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, lakini akalazimika kujiuzulu mwaka 2008 baada ya Kamati ya Bunge kuibua kashfa ya kuingia mkataba wa ufuaji umeme wa dharura na kampuni iliyokuwa haina sifa ya Richmond RDC, uamuzi ambao anasema aliufanya ili kuiokoa nchi.
Lowassa pia aliwahi kuwania urais mwaka 1995, lakini CCM ikampa nafasi Benjamin Mkapa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tatu.
Wakati Lowassa na timu yake wakiwa katika mikakati hiyo, makada wengine wa CCM ambao nao wanawania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho, pia wamejipanga kutangaza nia zao kila mmoja kwa wakati wake huku wanne kati ya hao wakitoa taarifa kutangaza nia katika siku mbili tofauti Jumapili na Jumatatu katika maeneo tofauti.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment