Aidha ameionya Urusi
kuzirekebisha mbinu zake kuhusu Ukraine ikiwa ingetaka kujiunga tena katika
kundi la mataifa tajiri ulimwenguni la G7. Kansela Merkel, ambaye ametekeleza
jukumu muhimu katika juhudi za amani kuhusu mzozo wa Ukraine, amesema Urusi
haina sababu ya kuogopa mahusiano ya karibu baina ya kundi hilo lenye nchi
wanachama 28 na mataifa sita yaliyokuwa sehemu ya muungano wa kisovieti.
Katika mazungumzo hayo ya
Riga, viongozi wa Umoja wa Ulaya watasisitiza nia yao ya kuyajenga mahusiano ya
kisiasa na kiuchumi na Armenia, Azerbaijan, Belarus, Georgia, Moldova na
Ukraine.
Mapema leo, Umoja wa Ulaya na
Ukraine zimesaini mkataba wa mkopo wa kiasi cha euro bilioni 1.8 katika juhudi
za kusaidia kuufufua uchumi wa nchi hiyo ulio na matatizo ya fedha.
Mpango huo unaiihitaji
Ukraine kuidhinisha msururu wa mageuzi zikiwemo hatua za kupambana na rushwa
ili kuyatatua matatizo ya kimuundo katika uchumi wake.
Katika mkutano huo wa Riga,
Umoja wa Ulaya pia umeahidi ruzuku ya euro milioni 200 ili kusaidia biashara
ndogondogo na za wastani katika nchi za Ukraine, Georgia na Moldova.
Merkel pia ameionya Urusi
kuwa isifikirie kurejea tena katika Kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda
ikiwa itaendelea kukiuka sheria ya kimataifa nchini Ukraine – kutokana na
kitendo cha kulinyakua jimbo la Crimea. Uwanachama wa Urusi ulilifanya kundi la
G7 kuwa G8 lakini washirika wake wakasitisha uwanachama wake mwaka jana huku wakisusia
kuhudhuria mkutano wa kilele ulioandaliwa mjini Sochi na Rais wa Urusi Vladmir
Putin kulalamikia hatua ya serikali ya Urusi kuwaunga mkono waasi wa mashariki
mwa Ukraine.
Mgogoro wa Ukraine, hata
hivyo, ulifichua migawanyiko mikubwa ndani ya umoja huo kuhusu namna ya
kushirikiana Urusi. Chini ya Mikataba yao ya Ushirikiano na Umoja wa Ulaya,
Georgia, Moldova na Ukraine zinaahidi kufanya mageuzi ya kisiasa na mashirika
ya kijamii yanayolenga kuzifanya nchi hizo kuwa na mifumo ya kisasa na kuweka
misingi ya kidemokrasia.
Matokeo yake ni kuwa nchi
hizo zitaweza kupata nafasi za kiuchumi katika Umoja wa Ulaya, ambao ni
mojawapo ya masoko makubwa kabisa ulimwenguni, na ushirikiano mkubwa wa
kisiasa. Moldova ilisaini mkataba na Umoja wa Ulaya wa raia wake kusafiri
katika nchi za umoja huo bila visa, lakini Umoja wa Ulaya unasema Ukraine na
Georgia bado zina kazi ya kufanya kabla ya kufikia kiwango kinachostahiki, hata
ingawa zimepiga hatua kubwa.
Mkutano huo wa kilele pia
unalenga kutatua masuala ya ndani katika Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu
aliyechaguliwa upya wa Uingereza David Cameron, atawasilisha suala lake la
kutathminiwa upya masharti ya uwanachama wa nchi yake katika umoja huo, kabla
ya kura ya maoni ya “kuwauliza wananchi ikiwa wanataka kubakia au kjiondoa,
aliyoahidi kuandaa mwaka wa 2017.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef.
Mhariri: Mohammed Khelef.
0 comments:
Post a Comment