Image
Image

Chama cha wanasoka kitathmini nafasi yake katika usajili.


Msimu wa usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la pili umeanza rasmi baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka 2014/15 na tayari klabu zimeanza kuonyesha uwezo wao wa kifedha kwa kusajili wachezaji kwa donge nono.
Wachezaji kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini na nje wanatangazwa kusajiliwa na klabu mbalimbali, hasa zile kubwa ambazo zina wadhamini na wafadhili wanaozifanya zionekane zina fedha.
Kipindi hiki pia ndicho kinachotawaliwa na habari za migogoro baina ya wachezaji na viongozi wa klabu kuhusu mikataba yao na stahiki zao. Wachezaji hulalamikia kutotekelezwa kwa mikataba yao kuhusu malipo mbalimbali, kama fedha za usajili, pango na wengine huingia kwenye migogoro na viongozi kwa kutaka fedha ili wasaini mikataba mipya.
Wakati mwingine migogoro hii huishia kwa wachezaji kupoteza haki zao kwa kuwa wengi wao hawana ufahamu wa kutosha kuhusu mikataba na pia hakuna chombo imara cha kuwatetea wakati wanaponyimwa haki zao kwenye klabu.
Suala hili linazidi kuwa kubwa kwa kuwa wachezaji hawana kimbilio na hivyo wanalazimika kuachia haki zao, na wengine kulazimika kuachana kabisa na mpira wa miguu kwa kuuona kuwa hauna maana kwao.
Hili si jambo zuri hata kidogo kwa kuwa linakatisha tama wachezaji na kufanya vijana ambao wana vipaji waamue kutafuta vitu vingine vya kufanya na hivyo kuwaacha wale tu ambao wanaweza kuvumilia kuporwa haki zao ndio waendelee kujishughulisha na mpira wa miguu.
Wakati huu tunashuhudia hayo, ni muda mzuri kwa wachezaji kutafakari kuhusu haki zao na wanawezaje kuungana ili wawe na chombo kimoja ambacho kitakuwa kikisimama imara kuwatetea pale wanapokuwa na matatizo na klabu zao.
Tunajua kuwa kwa sasa kuna Chama cha Wanasoka wa Tanzania (Sputanza) ambacho kina wajibu huo wa kuwasimamia wachezaji, lakini kinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na kutokuwa na fedha na pia kuwa sehemu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Sputanza imeshindwa kuonyesha umuhimu wake kwa wachezaji ambao nao wanashindwa kujihusisha nayo kwa kuona kuwa si muhimu.
Kwa maana hiyo ni muhimu kwa Sputanza kuanza kutafakari nafasi yake katika kusimamia na kutetea maslahi ya wachezaji, hasa kipindi hiki ambacho kinaonyesha wazi kuwa wachezaji wanahitaji msaada mkubwa wa watu wenye ufahamu wa masuala ya sheria na mikataba ili wasidhulumiwe haki zao.
Sputanza haitakiwi kusimamia wachezaji ambao ni wanachama wake tu, bali isimame kutetea wachezaji wote na ndipo wataona kuna umuhimu wa kujiunga na chama na hivyo Sputanza kuwa na wanachama wengi ambao watakifanya kiwe na nguvu zaidi.
Hatuhitaji kuwa na sheria au kanuni mpya kwa ajili ya kusimamia haki na maslahi ya wachezaji kwa kuwa tayari Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) lilishatengeneza kanuni imara ambazo zinaweza kusimamia haki za mchezaji popote pale alipo ulimwenguni.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment