Image
Image

Kisukari,saratani na moyo chanzo cha vifo duniani kote.

Magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo ya kisukari, moyo na saratani, yanazidi kuongezeka kwa kasi na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani kote.
Aidha, inakadiriwa kuwa kisukari pekee kimeathiri maisha ya watu takribani milioni 371 duniani kote huku asilimia 80 ya idadi hiyo ikiishi katika nchi zenye uchumi wa kati na maskini.
Nchini Tanzania, takribani watu tisa kati 100 wana ugonjwa wa kisukari na kwamba mtu mzima mmoja kati ya watatu, ana tatizo la shinikizo la juu la damu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hauson Rweumbiza, wakati wa semina ya siku moja iliyowashirikisha waandishi wa habari wa kutoka vyombo mbalimbali.
Lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuzungumzia magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.
Alisema gharama ya kukabiliana na magonjwa ya siyo ya kuambukiza duniani kote ni mabilioni ya dola na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa rasilimali finyu zilizopo.
"Kwa mwaka 2010, Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa jumla ya gharama zinazohusiana na kisukari zilifikia Dola bilioni 378 duniani kote na kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia Dola bilioni 490 ifikapo mwaka 2030,'' alisema.
Aliongeza kuwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania na zilizoendelea, pia hazina rasilimali za kutosha kutibu watu wote wanaobainika kuwa na kisukari.
Aliongeza kuwa jitihada za kukabiliana na tatizo hilo ni budi zikajikita zaidi katika mitazamo jumuishi inayolenga kukinga ili kupunguza kiwango cha magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii.
Alisema kwa kufahamu hilo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Taasisi ya Kisukari Tanzania pamoja na wadau wengine, imeandaa kitabu kwa lengo la kupunguza athari na matokeo mapya ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye jamii ya Watanzania.
Alifafanua kuwa kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha nyepesi, kinajumuisha taarifa muhimu na kumpa nafasi kila mtu kuchagua mtindo wa maisha utakaomwezesha kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa usioambukiza.
Aidha, aliwataka wananchi kuachana na uzushi ambao umekuwa ukitolewa na baadhi ya wafanyabiashara kuwa mayai ya kware hutibu ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na kuongeza kinga kwa watu wenye Ukimwi.
"Watu wapo kibiashara zaidi, mayai ya kware ni kama mayai ya kuku na bata na hayatibu kisukari, shinikizo la damu wala  kuongeza kinga kwa watu wenye Ukimwi," alisisitiza.
Hali kadhalika, aliwataka wagonjwa wa kisukari kuacha kutumia asali kwani wamekuwa wakilaghaiwa na wafanyabiashara kwamba ni mbadala wa sukari.
Naye Mratibu kutoka Taasisi ya Kisukari hapa nchini, John Gadina, alisema utafiti uliofanyika mwaka 2012, ulionyesha kuwa asilimia tisa ya Watanzania waligundulika kuwa na kisukari huku Wilaya ya Temeke ikiongoza.
Alisema ugonjwa huo umewakumba vijana na watu wenye umri mkubwa na kwamba serikali mpaka sasa imefikia kutoa huduma hiyo kwa asilimia 75 ambapo kila palipo na hospitali panakuwa na kitengo cha kutoa huduma za ugonjwa huo.
Alisema sababu ya Wilaya ya Temeke kuwa na wagonjwa wengi imetokana na ulaji kwa wingi wa vyakula vya nazi, chapati, wali pasipo kufanya mazoezi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment