Taarifa za Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC)
na Mkutano Mkuu zilikuwa zikitolewa na chama hicho kwenye mitandao yake
kabla hata ya kuzitangaza rasmi.
Tangu kuanza kwa mchakato wa mikutano hiyo, CCM
ilionekana kujiandaa vilivyo baada kutumia karibu njia kuu zote za
mitandao ya kijamii ikiwamo kurusha moja kwa moja matangazo ya Mkutano
Mkuu kupitia kiunganishi cha mtandao www.bit.ly/MkutanoMkuu.
Licha ya kuwa chama hicho kilikuwa na akaunti za
Facebook, Twitter, Youtube kwa muda mrefu, lakini kipindi hiki
zilionekana kuboreshwa na kutumika mara kwa mara kiasi hata cha kutoa
taarifa kabla ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuwatangazia
wanahabari.
Ikumbukwe kuwa matokeo ya majina ya wagombea wa
tano bora yaliwahi kutoka katika tovuti na akaunti ya Twitter ya chama
hicho mara tu baada ya Kamati Kuu kumaliza kikao huku nyuma Nape
akikwepa kuwaambia wanahabari.
Pia, matokeo ya tatu bora nayo yalitangazwa mapema
kupitia vyombo hivyo dakika 10 mapema kabla ya Nape kuwatangazia rasmi
wanahabari.
Hata hivyo, kasi ya vyombo hivyo kutangaza kile
kinachoendelea kwenye mchakato huo ilitaka kuingia doa pale walipoandika
kwenye ukurasa wao Twitter wenye jina @ccm_tanzania matokeo ya mshindi
wa kinyang’anyiro cha urais na kuchanganya asilimia za kura walizopata
wagombea Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali.
“Tunaomba radhi. Matokeo halisi ya kura za
wagombea kutoka Mkutano Mkuu ni: Mh John Magufuli asilimia 87, Balozi
Amina Ali asilimia 10, Dk Asha Migiro asilimia 3,” CCM ilisahihisha
twiti yao baada ya kuandika kuwa Dk Migiro alikuwa amepata asilimia 10
na Balozi Amina asilimia 3.
Pia, CCM ilitumia nguvu kubwa kutangaza akaunti
zake kwa kuziwezesha zionekane kwenye mtandao kwa kutumia reli
#KaribuDodoma ambayo kwa mara ya kwanza ilionekana kuongoza kutajwa
kwenye mtandao wa Twitter nchini.
Kwa kawaida, kuwezesha akaunti au neno lionekane
mara kwa mara katika mitando ya kijamii unatakiwa kulipia fedha kutokana
na mahitaji yako au watu waitaje mara kwa mara akaunti au neno hilo
mtandaoni.
Awali, gazeti hili liliwahi kuzungumza na Nape juu
ya mikakati ya kutumia Tehama wakati wa Uchaguzi Mkuu na kubainisha
kwamba CCM ingetumia akisisitiza kuwa hiyo ni moja tu ya njia za
kuwaunganisha na wananchi wenye uwezo huo lakini nguvu kubwa itaendelea
kwenye mikutano ya hadhara inayowafikia hadi wananchi wa vijijini.
0 comments:
Post a Comment