Image
Image

Lipumba azidi kubanwa mahakamani.

Ofisa Operesheni wa Polisi Temeke, Muhudhnwari Msuya ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alikiri kupokea barua ya polisi iliyowazuia kufanya maandamano na mkutano Mbagala Zakhem, lakini alikaidi.
Shahidi huyo wa upande wa mashtaka alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha katika kesi inayomkabili Lipumba na wafuasi wake 30.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola alidai kuwa Januari 27, mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Polisi Temeke, Sebastian Zacharia alifika karibu na Ofisi za CUF, Mtaa wa Boko Temeke, mkabala na Hospitali ya Temeke na Benki ya NMB na kuelezwa hali ilivyokuwa.
Msuya alidai kuwa alimpa taarifa Lipumba kuhusu mkusanyiko wa watu uliokuwa na dalili za kuanzisha maandamano.
Alidai kuwa ilipofika saa saba mchana, alimuona Lipumba na wanachama wake wakiimba nyimbo zenye maudhui ya CUF, huku wakiwa na bendera na mabango wakielekea yalipokuwapo magari ya polisi.
“Walipotufikia, Lipumba alishuka kwenye gari na kumuomba Kamanda Zacharia awaruhusu yeye pamoja na wafuasi wake kwenda Mbagala.
“Afande Zacharia alimuuliza Lipumba kama alipata barua ya polisi ya kuzuia maandamano na mkutano iliyoandikwa Januari 26, mwaka huu. Lipumba alikiri kuiona, lakini akasisitiza yeye na wafuasi wake lazima waende Mbagala.”
Aliendelea kudai kuwa Lipumba alishauriana na wafuasi wake na wao kama polisi walishauriana jinsi ya kuwazuia.
“Baada ya kushauriana, tulibaini kuwa katika mazingira waliyokuwapo ya hospitali na Benki ya NMB katika eneo hilo, tuliwacha wapite kwa vile ingekuwa hatari kama tungeanza kuwazuia hapo.”
Alisema baada ya muda, Lipumba na wafuasi wake na magari yao walipita walipokuwapo askari kuelekea Mbagala, hivyo polisi wakaamua kupita njia ya mkato ya Tandika Magengeni na kuwazuia katika eneo la Mtoni Mtongani.
“Tungepita barabara waliyopita wao tungeshindwa kuwazuia kwa sababu tungekuwa nyuma yao,” alisema.
Msuya alidai kuwa wakiwa hapo, waliyaegesha magari yao barabarani na baadaye Lipumba na wafuasi wake walifika na kuongea na Zacharia.
Alidai katika maongezi yao, Lipumba na wafuasi wake walitaka kuruhusiwa kwenda kwenye mkutano Mbagala Zakhem.
Alisema walisogea katika mzunguko wa barabara katika eneo la Mtongani, lakini bado wafuasi wa Lipumba walisisitiza kutaka kwenda Mbagala Zakhem.
Kamanda Zacharia alimuagiza OCD Ramia Mganga kusoma ilani, ambayo wakati huo ilikuwa imekwishanyooshwa mara tatu na kisha kurudiwa tena, huku msisitizo ukiwa ni kuwataka kuondoka katika eneo hilo.
Aliwataka waondoke vinginevyo ingetumika nguvu, lakini pamoja na amri hiyo, wafuasi hao waliendelea kukaidi, ndipo nguvu ya dola ilipotumika.
Shahidi huyo akihojiwa na Wakili wa Lipumba na wafuasi wake, Twaha Taslima alidai kuwa Lipumba aliomba kwenda Mbagala kuahirisha mkutano. Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa tena leo mahakamani hapo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment