Image
Image

Muda wa nyongeza wa kujiandikisha utumiwe vizuri.

Jana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitangaza kuongeza siku nne zaidi za uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa mfumo wa utambuzi wa alama za mwili (Biometric Voters Registration – BVR) katika mkoa wa Dar es Salaam. Awali uandikishaji wa wapiga kura katika mkoa huo ulikuwa ni wa siku 10 na ungemalizika leo.

Uamuzi wa kuongeza muda hapana shaka ni mwitikio wa kilio cha wadau wengi wa uchaguzi mkuu kwamba wananchi wengi wa mkoa huo walikuwa hawajajiandikisha licha ya taarifa ya Nec kuonyesha kuwa hadi juzi, waliokuwa wamekwisha kuandikishwa ni wapigakura milioni 1.7 kati ya lengo la kuandikisha wapiga kura milioni 2.9 kwa mkoa huo.

Kimahesabu hadi siku mbili zinabakia kukamilika kwa kazi ya uandikishaji kwa kufuata ratiba ya awali, Nec ilikuwa imefanikiwa kufikia lengo lake kwa walao asilimia 58.6. Mafanikio haya siyo mazuri sana hata kama kungefurika maelfu ya watu vituoni kwa siku hizo mbili. Isingeliwezekana kuandikisha watu milioni 1.2 kwa siku mbili tu. Uwezo huo haupo.

Ndiyo maana tunachukua fursa hii kuipongea Nec kwa kuwa sikivu, hivyo kuongeza muda wa kuandikisha wapiga kura katika mkoa wa Dar es Salaam kwa siku nne zaidi. Tunaamini hatua hii itakuwa ni fursa murua kwa wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi zaidi ili ifikapo Jumanne ya Agosti 4, mwaka huu walao lengo liwe limefikiwa na ikiwezekana kuvuka.

Pamoja na usikivu wa Nec, sisi bado tuna maswali, hoja na tashwishi nyingi kwamba bado kuna mambo mengi hayajakaa sawa katika mchakato mzima wa uandikishaji wapiga kura. Kubwa ya yote ni uwezo wa mashinde za BVR na pengine hata uwezo wa waandikishaji wenyewe.

Tangu kuanza kwa kazi ya uandikishaji wapigakura Februari 23, mwaka huu mkaoni Njombe kumekuwa na changamoto za kiufundi ambazo zingali zinaendelea kuwako hata sasa katika mkoa wa Dar es Salaam licha ya uzoefu ambao umepatikana katika mikoa mingine yote ya nchi ambako kazi hii imekamilika.

Kuzimika ovyo kwa mashine hizi ni mambo ya kawaida kabisa. Katika baadhi ya vituo kuna mashine zinazimika hadi nusu saa. Zikiwashwa zinachukua muda mrefu sana kuwaka huku wananchi wakitaabika juani wakisubiri kuandikishwa. 
Maeneo mengi katika mkoa wa Dar es Salaam kumekuwa na msongamano au tuseme misururu mirefu ya wananchi wanaodamka alfajiri na mapema wengine hadi saa tisa, ili kuwahi kupata namba kwenye vituo. Wapo wanaoandikishwa baada ya kusota vituoni siku mbili hadi tatu. 

Tunafikiri, Nec ilikuwa na uwezo wa kuwa na vituo vingi kadri iwezekanavyo na kuongeza mashine za BVR nyingi zaidi kwa kuwa zipo za kutosha kwani maeneo mengine ya nchi kazi ya uandikishaji imekwisha kukamilika.

Kwa kutambua ukweli huo, haitoshi tu kwa Nec kuongeza muda wa siku nne ili wananchi zaidi wajiandikishe kama idadi ya mashine itaendelea kubakia ilivyo sasa. Nguvu kubwa zaidi ya vifaa na watendaji vituoni inatakiwa ili kufanikisha kazi hii muhimu.

Ni fedheha kwa wananchi kudamka alfajiri kiasi hicho, lakini mwishoni washindwe kujiandikisha kwa sababu tu ya uhaba wa mashine vituoni, au kwa sababu tu zinazimika zimika kila mara kwa sababu yoyote ile. Nec inapaswa kuondoa kasoro hii.

Wananchi wamesikia tamko la Nec kwamba sasa vituo vya kuandikisha wananchi vifunguliwe kuanzia saa 1:00 asubuhi na kuendelea kufungwa saa 12:00 jioni, lakini swali gumu ambalo halina majibu ni je, makarani hao wanaofanya kazi ya kuandikisha watu watafika vipi kwenye vituo vyao? Je, Nec imeweka utaratibu gani wa usafiri wa kuwawezesha kufika kwenye vituo? Tunajua wapo wanaokaa mbali na vituo vyao, lakini pia maeneo mengine ambako vituo vimewekwa hakuna usafiri wa umma. Huko kote kunahitaji nguvu ya Nec kuwezesha kazi kuanza saa 1:00 asubuhi.

Pamoja na changamoto hii kwa Nec, tunaamini kwamba wakazi wa Dar es Salaam ambao hawajajiandikisha kwa sababu yoyote ile nao watawajibika kutumia siku hizo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili ifikapo Oktoba 25, mwaka huu watumie haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wao. Ni matumani yetu kwamba Nec wataendelea kutafutia ufumbuzi changamoto hizi kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine wananchi wataendelea kujitokeza kwa wingi zaidi kujiandikisha katika siku hizo nne zilizoongezwa na hatimaye watumie haki yao ya kidemokrasia Oktoba 25, mwaka huu kuchagua madiwani, wabunge na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment