Image
Image

LUBUVA - Ni Marufuku Kusafirisha Masanduku ya Kura*Tume Yasisitiza Matokeo Yatatangazwa Vituoni.


MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kura zote za urais, ubunge na udiwani, zitahesabiwa katika vituo vya kupigia kura na matokeo yote kutangazwa hapo hapo na ni marufuku kusafirisha masanduku ya kura kama ilivyokuwa zamani.
Jaji Lubuva aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano na wawakilishi wa walemavu   kujadili namna bora ya wao kushiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa  mwaka huu ni marufuku kuhamisha masanduku ya kura kwa sababu vituo vya kupigia kura vitabadilika kuwa vituo vya kuhesabia kura baada ya upigaji kura kumalizika.
“Kura zote za urais, ubunge na udiwani zitahesabiwa katika kila kituo na matokeo yatabandikwa vituoni hapo hivyo sijui wanaosema kura zitaibiwa zitaibiwaje,” alisema JajiLubuva na kuongeza:
“Baada ya matokeo kubandikwa katika kila kituo yatapelekwa katika kata husika   kujumlishwa na hapo pia yatabandikwa.
“Mshindi wa udiwani atatangazwa hapo na yale ya ubunge na urais yatapelekwa jimboni ambako yatajumlishwa na mshindi wa ubunge atatangazwa na kukabidhiwa cheti huku ya urais yakipelekwa makao makuu ya Tume.
“Matokeo ya urais yatabandikwa katika kila jimbo na fomu ile ya matokeo itaskaniwa na kutumwa moja kwa moja makao makuu ya tume kwa kupitia mkongo wa mawasiliano wa taifa badala ya simu za mkononi kama ilivyokuwa awali,” alisema Lubuva.
Alisema njia hiyo  itasaidia matokeo kufika kwa haraka kama inavyotakiwa na baada ya tume kupokea matokeo hayo itakuwa ikiyatangaza moja kwa moja kupitia luninga na redio.
Jaji Lubuva alisema  njia nyingine iliyoandaliwa ya kutuma matokeo ni kwa nukushi (fax) ambako  halmashauri zote nchini zimepatiwa vifaa vitakavyoziwezesha kuyatuma matokeo haraka.
Alisema hatua ya tume kutangaza matokeo hayo kupitia luninga na redio itasaidia wananchi kulinganisha matokeo watakayokuwa nayo na yatakayokuwa yanatangazwa na tume.
Kutokana na hali hiyo alivishauri vyama vya siasa viache kauli za kuwataka wafuasi wao wasiondoke vituoni baada ya kupiga kura kwa vile  hakuna kura zitakazoibiwa.
“Sioni haja ya vyama kusema vinalinda kura kwa sababu kura zote zinabaki vituoni na zitahesabiwa palepale tofauti na zamani ambako zilikuwa zikipelekwa kata na jimboni kuhesabiwa,” alisema.
Jaji Lubuva pia alivitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia majukumu ya Tume hiyo ikiwamo kuhoji mabadiliko ya watendaji yanayofanywa ndani ya taasisi hiyo.
“Navishauri vyama vya siasa viache kuingilia majukumu ya Tume, haviwezi kutuchagulia na kutuambia pale weka karani fulani hapa fanya hivi… waache kuingia jikoni wasubiri chakula kipikwe watakula kwa haki wala wasiogope,” alisema.
Ametoa kauli hiyo  siku chache baada ya vyombo vya habari kumnukuu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akisema Mkurugenzi wa Tehama wa Tume hiyo, Sisti Cariah ameondolewa katika nafasi hiyo huku akihusisha mabadiliko hayo na maandalizi ya  kuiba kura.
Hata hivyo NEC ilikanusha taarifa hizo   ikisema hakuna mtu yeyote aliyehamishwa katika idara zake zote isipokuwa wakuu hao wa idara walichelewa kuwasilisha picha zao ndiyo sababu  hawajaingizwa katika orodha iliyomo katika tovuti ya Tume. 
Jaji Lubuva alisema daftari la mwisho la wapiga kura litakamilika baada ya wiki mbili hadi tatu na wapiga kura watapata fursa ya kulihakiki kwa siku nane kabla ya uchaguzi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment