Image
Image

Mungu awalaze pema waliofariki katika mkanyagano Hijja Makkah.

Kuna taarifa za kusikitisha kuwa mahujaji watano kutoka Tanzania ni  miongoni mwa waliofariki katika tukio la mkanyagano kwenye Mji  Mtakatifu wa Makka, nchini Saudi Arabia.
Kwa ujumla, watu 717 wameripotiwa kufa na wengine zaidi ya 800  kujeruhiwa katika tukio hilo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Kimataifa jana ilieleza kuwa Watanzania hao walifariki wakati  wakiendelea na ibada ya Hijja kwenye eneo la Mina, ndani ya Mji  Mtakatifu wa Makka.
Hakika, huu ni msiba mkubwa. Sisi tunaungana na Watanzania wengine  kuwapa pole wafiwa na pia kuwatakia kheri wote waliojeruhiwa ili  wapate nafuu haraka.
Ni imani yetu kuwa serikali yetu, kwa kushirikiana na  Saudi Arabia,  itaendelea kufanya kila linalowezekana ili taarifa kamili ziendelee  kupatikana kuhusiana hatima ya mahujaji wetu. Taarifa zilizopo ni  kwamba mwaka huu, Watanzania takriban 2,700 wamekwenda kutekeleza  ibada hiyo muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo. Mbali na kwenda  kuhiji Makka, nguzo nyingine kati ya tano za Uislamu ni kutoa  shahada, kusimamisha swala, kutoa zaka na kufunga (swaumu) Ramadhani.
Sisi tunaamini kuwa muhimu zaidi kwa sasa ni kwa kila mmoja kuendelea  kuwaombea mahujaji wetu waliosalimika ili mwishowe warejee nchini  wakiwa bukheri wa afya.
Aidha, ni muhimu pia kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili awajaalie  pepo yenye daraja ya juu mahujaji wetu waliopatwa na umauti, hasa kwa  kutambua kuwa kilichowapeleka Makka siyo kitu kingine bali ni  kujinyenyekeza mbele za Allah (Mwenye Mungu) ili mwishowe wapate  radhi zake.
Katika kipindi hiki, ni imani yetu kuwa ndugu, jamaa na marafiki wa  marehemu watajitahidi kuwa na subira kadiri wawezavyo. Ni kwa sababu,  kwa mujibu wa mafundisho, kila nafsi itaonja umauti. Na hili  lililotokea ni sehemu ya mtihani ambao siri ya kufaulu kwake  kwategemea kiwango cha subira kwa kila mmoja wao. 
Pamoja na yote, tunaamini kuwa baada ya shughuli za uokoaji na  mazishi kukamilika, serikali ya Saudi Arabia itahakikisha kuwa  uchunguzi wa kina unafanyika ili mwishowe kubaini chanzo cha  mkanyagano na kuchukua hatua sahihi za kuzuia majanga ya aina hii.
Kinachotakiwa kuangaliwa na waandaaji ni taratibu za kutoa fursa kwa  kila hujaji kutekeleza ibada ya Hijja akiwa salama. Rekodi  zinaonyesha kuwa vifo vya aina hii vimewahi pia kutokea mara kadhaa  hapo kabla katika tukio hilo linalokutanisha watu wengi zaidi kwa  wakati mmoja duniani, huku mwaka huu likihusisha mahujaji takriban  milioni mbili. 
Kwa mfano, mwaka 1990 walikufa mahujaji 1,426, mwaka 1994 (watu 270)  na pia mwaka 2006 walikufa watu 360. Hali hii inapaswa kuzuiwa kwa  kupitia upya taratibu za kuwezesha waumini kutekeleza ibada hii  muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo.
Mungu awalaze pema peponi mahujaji wote waliotangulia mbele ya haki.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment