Mapendekezo ya nauli hizo yanatazamiwa kutumiwa na kampuni ambayo
itatoa huduma ya usafiri wa umma katika njia na miundombinu ya Dart
katika kipindi cha mpito.
Kiwango cha juu kilichopendekezwa na Dart ni Sh. 900 ambacho
kitahusu zaidi safari katika njia za pembezoni na njia kuu zilizojengwa
kwa ajili ya kutumiwa na mabasi hayo.
Pia viwango vingine vilivyopendekezwa ni Sh. 700 na Sh 500, viwango
vinavyotegemea zaidi njia inayotumiwa na wananchi. Kufuatia mapendekezo
hayo, Sumatra imetangaza kuwa itakaa na wadau kujadiliana nayo juu ya
mapendekezo hayo ya nauli kama yalivyotolewa na Dart.
Hata hivyo, mapendekezo hayo tayari yamezua manung’nuko kutoka kwa
wananchi ambao wanaamini kuwa kiasi kilichopendekezwa ni kikubwa kuliko
hali halisi ya kiuchumi. Ni dhahiri kwamba usafiri wa mabasi ndiyo
tegemeo kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini katika Jiji la Dar es
Salaam, hivyo kupanga kiasi kikubwa cha nauli kwa vyovyote vile
kitawaathiri kwa kiasi kikubwa.
Tunaiomba serikali iangalie suala hili la nauli kwa kuwa tunaamini
kwamba uanzishwaji wa mradi wa Dart ulikuwa na nia njema ya kuwapunguzia
adha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na kupunguza foleni.
Mradi wa Dart ulianzishwa kufuatia mkopo wa Dola milioni 290 za
Marekani kutoka Benki ya Dunia ambao Serikali ya Tanzania itatakiwa
kuulipa. Kwa maneno mengine ni kwamba fedha za umma zitatumika kulipa
mkopo wa mradi huo.
Kwa msingi huu, wananchi wengi walikuwa na matumaini kwa kuwa fedha
zinazotumika ni za mlipa kodi, kutakuwa na nafuu tofauti na usafiri wa
mabasi ya daladala yanayomilikiwa na sekta binafsi. Lakini katika hali
ya kushangaza, mapendekezo ya Dart yanatoa picha kuwa mradi huu
unaelekea kujiegemeza katika kutengeneza faida zaidi badala ya kusaidia
wananchi wa kipato cha chini waliokuwa wakiisubiri kwa hamu huduma hii.
Uzoefu unaonyesha kwa mifano ya nchi mbalimbali duniani kuwa pale
serikali inapoweka mkono katika uendeshaji wa usafiri wa umma, nauli
zake ni nafuu.
Kitendo cha Dart cha kutaka kutoza nauli za kiasi kikubwa,
kitawaumiza wananchi wa kawaida ambao katika wakati huu tayari wana hali
ngumu ya maisha ikichangiwa na uduni wa uchumi unaochangiwa kuporomoka
kwa thamani ya Shilingi kwa kiasi kikubwa kutoka kwa dola siku za
karibuni.
Ni matumaini yetu kuwa Sumatra itasikiliza kilio cha wananchi walio
wengi na kuhakikisha kuwa wanapanga bei za usafiri wa mabasi ya Dart
zinazoendana na uhalisia wa maisha ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wa
kipato cha chini.
Aidha, kwa Dart kupendekeza kiwango hicho cha juu cha nauli,
kunaweza kuamsha kilio kutoka kwa wamiliki wa mabasi ya daladala ambao
kila mara nao wamekuwa wakililia kupandishwa kwa nauli kwa kisingizio
cha kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Tunaomba wadau kujitokeza kwenye mkutano wa kujadili mapendekezo
hayo ya nauli za mabasi ya Dart ulioandaliwa na Sumatra ili upatikane
muafaka utakaokidhi matakwa ya wananchi wanaolilia usafiri wa uhakika na
wa bei nafuu.

0 comments:
Post a Comment