Image
Image

Lowasa:Tanzania bila CCM inawezekana.

Zikiwa zimebaki siku 12 uchaguzi mkuu kufanyika, mgombea wa urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa, amepokelewa mkoani Mara kama mfalme, huku baadhi ya wananchi wakifagia na kudeki barabara ili aweze kupita.
Wananchi hao walianza kuwasili kwenye uwanja wa mkutano kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kumsikiliza mgombea huyo.
Hayo yalifanyika jana mjini Musoma kwenye uwanja wa Mkendo,mkoani Mara.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa kampeni, Lowassa alisema Tanzania bila CCM inawezekana na kuwataka wananchi wapige kura kuiondoa madarakani.
"Nasema hivi, Tanzania bila CCM inawezekana pigeni kura nyingi tuiondoe," alisema.
Aidha, Lowassa alisema iwapo ataingia madarakani serikali yake itahakikisha inamalizia kujenga Hospitali ya Rufaa Kwangwa ambayo haijamaliziwa kujengwa kwa muda mrefu.
"Nikiingia madarakani nitahakikisha hospitali hiyo inakamilika na wananchi wanapata huduma," alisema.
Aidha, alisema atahakikisha anafuta ushuru wote wa mazao kwa wakulima.
"Nitaondoa kodi na mkulima atapata uhuru wa kuuza mazao yake katika maeneo yote atakayotaka," alisema. 
NYERERE
Mgombea wa Ubunge Jimbo la Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere, alisema iwapo kura zingepigwa leo (jana), Lowassa angeshinda kwa asilimia 90 kwa sababu watu wanahitaji mabadiliko.
Alisema CCM imepoteza muelekeo,  imeshusha pumzi ambayo inakatika muda wowote kuanzia sasa.
"Walipokuja CCM kufanya kampeni kwenye uwanja huu hawakuweza kuujaza kama tulivyojaza sisi...nina imani na watu wangu," alisema.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema maisha ya watu yamekuwa ya shida zaidi ikiwa ni pamoja na gharama za maisha kupanda kwa sababu ya CCM.
"Wapo wakina mama Watanzania wakitaka kwenda kujifungua wanaambiwa wakatafute glovu za kuvaa manesi ndiyo wajifungue, wapo wazee wa Kitanzania ambao wametumikia nchi hii kwa miaka 60 wanashindwa kutibiwa bure," alisema.
"CCM imeshindwa kutimiza kile ilichoahidi kwa wananchi ni lazimia iondoke madarakani."
Alisema hawawezi kuwa na chama ambacho kimekaa madarakani na hakiwajali wananchi.
"Kimewatesa Watanzania...kinachotakiwa sasa ni wao kuondoka madarakani na kutuachia nchi yetu," alisema.
MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema hakuna ufisadi mkubwa uliofanywa na CCM kama kuua Azimio la Arusha.
"Nashangaa CCM wanapanda kwenye majukwaa na kuanza kumtukana na kumnyooshea kidole Lowassa wakati wenyewe siyo wasafi, hakuna matumaini ndani ya CCM, wamepoteza dira na muelekeo,"alisema na kuongeza kuwa:
"CCM aliyoiacha Hayati Julius Nyerere haipo tena, hii iliyobaki ni CCM ya wala rushwa, wabadhilifu na mafisadi."
Alisema kama Lowassa angekuwa fisadi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) isingemruhusu kugombea urais kupitia Chadema.
"Nec ilitoa muda kwa watu kuweka pingamizi lakini hakuna mtu yeyote aliyeweka pingamizi," alisema.
Aidha, aliwashangaa wana CCM wanaposimama kwa watu na kujiita wasafi wakati ni wachafu na ni mafisadi ndani ya chama.
"Vigogo wakubwa waliopo ndani ya CCM ndiyo wanaosafirisha meno ya tembo," alisema.
Aidha, alisema Rais Jakaya Kikwete ameiharibu Tanzania kwa kuanzisha mradi wa Katiba ambao umekula mabilioni ya fedha za Watanzania.
Alisema mgombea wa CCM, John Magufuli hawezi kuiongoza Tanzania kwa sababu hata ubalozi wa nyumba 10 haujui.
OLE-MEDEYE
Naye, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dk. Goodluck Ole-Medeye, alisema iwapo Lowassa ataingia madarakani atapitia upya mikataba ya madini na gesi ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hizo.
"Wachimbaji watawezeshwa kwa kumilikishwa vitalu kwa ajili ya kuchimba madini," alisema.
Aidha, alisema wananchi ambao ardhi yao imechukuliwa na serikali bila kulipwa fidia, maeneo hayo yatafanyiwa tathmini na kulipwa fidia.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment