Image
Image

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dk.Magufuli ataja nguzo 10.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Dk. John Magufuli, ameteua jopo la wataalamu wa kila nyanja litakalochunguza na mwishowe kutoa mapendekezo ya kitaalamu katika maeneo 10 ya ahadi zake ili kufanikisha mabadiliko ya kweli pindi atakapofanikiwa kuingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika  Oktoba 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, January Makamba, alisema jopo hilo linahusisha wanataaluma na wataalamu wazalendo walio huru na tena waliobobea katika nyanja zote muhimu zikiwamo za uchumi, biashara, utawala na sheria kwa ajili ya maandalizi ya kufanya mabadiliko makubwa kuanzia siku ya kwanza atakayoingia madarakani. 
Wataalamu hao wanatoka katika taasisi za elimu ya juu, asasi za kiraia na sekta binafsi. Akifafanua, Makamba alisema jukumu kubwa la jopo hilo ni kuangalia namna mabadiliko ya kweli yatakavyofanikishwa kwa vitendo pindi Magufuli atakapoingia madarakani.
Kwa mujibu wa Makamba, eneo la kwanza litakaloangaliwa na jopo hilo ni kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi, ikiwamo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili (rais) atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa. 
Pili, ni kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
Makamaba alieleza zaidi kuwa eneo la tatu litakalofanyiwa kazi na jopo hilo ni kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi, na pia ufanisi katika Serikali.
Eneo la nne ni kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa na eneo la tano muhimu ni kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha Sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania.
"Eneo jingine ni kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa," alisema Makamba wakati akitaja jukumu la sita la jopo hilo.
Kadhalika, wajumbe wa jopo hilo watakuwa na jukumu la saba la kupendekeza miundo na idadi ya wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.
Makamba alitaja jukumu la nane la jopo la wataalamu kuwa ni kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi ili (Magufuli) aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.
Eneo la 9, ni kutengeneza rasimu ya mpango kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa (Magufuli) kwenye kampeni, hasa juu ya  upatikanaji wa ajira kwa haraka na pia umeme wa uhakika.
Mjumbe huyo wa kampeni ya Magufuli alitaja eneo muhimu la kumi litakalochunguzwa na kutolewa mapendekezo na wataalamu kuwa ni  kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini.
Maeneo yote hayo yanapaswa kufanyiwa kazi kitaalamu kwa sababu, "Dokta Magufuli ameazimia kuanza kazi mara moja kwa bidii kubwa na maarifa mapya," alisema Makamba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
MWINYI, MKAPA KUONGEZA NGUVU
Katika hatua nyingine, Makamba alisema marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi wa awamu ya pili na Benjamin Mkapa wa awamu ya tatu wataungana na viongozi wengine mbalimbali wa CCM watakaoongeza nguvu kampeni zao kwa kuzunguka nchini kufanya mikutano mbalimbali kwa ajili ya wagombea wao akiwamo Dk. Magufuli.
Alisema Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, ameanza ziara ya kampeni katika majimbo 64 huku Mkapa, Mwinyi na viongozi wengine wakitarajiwa kuanza safari ya kuzunguka nchi nzima na watatumia helikopta nne kufanikisha kazi hiyo.
Alisema Dk. Magufuli na Samia Suluhu wataendelea kutumia usafiri wa gari hadi mwisho wa kampeni isipokuwa pale tu itakapobidi ndipo watatumia njia nyingine za usafiri.
Akieleza zaidi kuhusu mwenendo wa kampeni wa Magufuli, Makamba alisema kuwa hadi sasa, Magufuli ameshaifikia mikoa 22, majimbo 203 na kufanya mikutano mikubwa rasmi 240 na mikutano mingine isiyo rasmi 865, mingi ikiwa ni baada ya kusismamishwa na wananchi wakati akiwa njiani. Hadi sasa, akitumia usafiri wa gari, ameshatembea Kilomita 31,467 za barabara kuu na barabara za kawaida.
Katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, Magufuli anatarajiwa kuchuana na wagombea wengine saba, ambao ni Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD; Janken Kasambala wa NRA, Fahmy Dovutwa wa UPDP, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashim Rungwe wa Chaumma na Maximillian Lymo wa TLP. 
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment