Image
Image

Dk.Shein na Maalim Seif wajichimbia kupata muafaka*CCM yakanusha Maalim kuapishwa.

Mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar, yameendelea tena jana Ikulu mjini hapa.

Mazungumzo hayo yaliyowajumuisha viongozi watano wa kitaifa akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais,Maalim Seif Sharif Hamad, yalichukuwa takriban saa sita.

Mazungumzo hayo yalianza saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni huku kukiwa hakuna taarifa zozote zilizopatikana kilichofikiwa katika mazungumzo hayo.

Bado vikao hivyo vya mazungumzo vimekuwa na usiri mkubwa licha ya kuenea kwa taarifa zisizo rasmi na  mitaani zimepewa jina la `Dripu.'

Viongozi wengine walihudhuria mazungumzo hayo jana ni Marais wastaafu Amani Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Vikao hivyo vimekuwa na usiri mkubwa ambapo hata viongozi wa vyama vikuu vya siasa vinavyohusika na mgogoro wa uchaguzi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF), vimeeleza havielewi kilichozungumzwa ndani ya vikao hivyo.

Chanzo cha kuzuka mgogoro huo ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu  kwa madai kuwa haukuwa wa huru na haki.

                                              CCM: Hatujaridhia Maalim Seif kuapishwa.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekanusha habari zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa kimeridhia mgombea urais wa visiwa hivyo kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif  Hamad, kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema taarifa zinazosambazwa mitandaoni na kumnukuu yeye akisema kuwa CCM imeridhia Maalim Seif apewe urais ni uongo kwani hakuna kitu kama hicho.

Alisema suala la kurudiwa uchaguzi ni jambo la lazima baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kufutwa na kutangazwa rasimi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu kama sheria inavyotaka.

Vuai alisema mshindi wa uchaguzi wa Zanzibar ataapishwa na kuwa Rais baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na siyo vinginevyo na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za uongo zinazosambazwa katika mitandao ya jamii kwa malengo maalum.

Vuai alisema CCM imechukua hatua za kuripoti katika vyombo vya sheria ili watu waliosambaza uzushi huo katika mitandao ya jamii wasakwe na kuchukuliwa hatua za sheria.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment