Image
Image

Kwa juhudi hizi za Rais Magufuli kusafisha uozo ziungwe mkono bila hiyana.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imejipambanua katika harakati zake za kurudisha uadilifu katika nchi na kukabiliana kwa nguvu zote na rushwa na ufisadi.

Pamoja na ukweli kuwa maadui wa taifa letu wanaojulikana ni ujinga, umaskini na maradhi, lakini matatizo ya rushwa na ufisadi kwa kiasi kikubwa nayo yamelitafuna taifa letu katika miaka ya karibuni.

Wananchi wengi wamekuwa na hasira na tatizo la rushwa na ufisadi ambalo baadhi ya watendaji wetu wameligeuza kama sehemu ya maisha ya kila siku.

Jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa ubabaishaji, ufisadi na rushwa, vimeshika kasi na kufanya kila mtu akishika dhamana ya serikali, basi ajenda yake ya kwanza ni kufanya maovu hayo.

Hata hivyo, siku chache baada ya kuchaguliwa Rais Magufuli, ameanza kazi ya kusafisha uozo katika taasisi mbalimbali za serikali.

Tayari juhudi zao zimezaa matunda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako hivi karibuni vilipelelekwa vitanda vipya na dawa.

Operesheni yao ya karibuni kabisa ni ile ya kukabiliana na tatizo la rushwa na ukwepaji kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Serikali imegundua upotevu wa makontena na kuanza uchunguzi wa kukabiliana na watendaji wanaojihusisha na masuala ya kuikosesha serikali mapato yake.

Hatua hii ya serikali ni ya kupongezwa kutokana na ukweli kuwa kama Rais Magufuli ataendelea na kasi hii, basi Tanzania itegemee maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Ni ajabu kuona Tanzania yenye rasilimali nyingi bado inahesabiwa kati ya nchi maskini duniani tofauti na nchi kama Singapore inayotegemea zaidi bandari yake kwa ajili ya kutengeneza pato la taifa.

Kutokana na vitendo vya baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali kujihusisha na vitendo vya ubabaishaji, rushwa na ufisadi ilifikia hatua ya watu wa taifa hili kuona vitendo hivyo viovu ni sehemu ya maisha yetu.

Hali hiyo ilitokana na ukweli kuwa vigogo walikuwa hawaguswi pale zinapotokea tuhuma kubwa za ufisadi.

Ilifikia hali ya kuzoeleka kuwa mtu anapoharibu sehemu moja basi anahamishiwa sehemu nyingine.

Wakati hayo yakitokea, raia wa kawaida hali ilikuwa tofauti kwani wengi wao kwa miaka mingi walijikuta wakiswekwa ndani tena kwa makosa madogo ya kudokoa simu n.k.

Bila shaka hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano zitasaidia kurudisha heshima ya serikali mbele ya jamii.

Katika miaka ya karibuni heshima ya serikali ilishuka kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana kulikuwa kuna kejeli nyingi dhidi ya hatua zake mbalimbali.

Mathalani, magari ya kifahari aina ya mashangingi yalipachikwa jina la `Kilimo Kwanza’ ikiwa ni sera ya serikali ya awamu ya nne.

Mathalan, wakati ilipoibuka kashfa ya wizi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ya Benki Kuu mwaka 2006 ulitoka mwongozo wa serikali wa kutaka watuhumiwa kurudisha fedha hizo ili wasamehewe.

Ilifikia hata kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa vyombo vya dola kunukuliwa akidai kuwa wezi hao wa Epa walikuwa hatari mno kiasi cha kuangusha serikali.

Inapofikia hatua vyombo vya dola kugwaya kukabiliana na matatizo ya rushwa na ufisadi, ni ishara ya wazi ya kutamalaki kwa vitendo hivyo viovu kwenye taifa.

Ndiyo maana tunaomba wananchi na watendaji wa serikali waunge mkono kampeni ya serikali ya awamu ya tano ya kusafisha uoza katika jamii ili nchi ipige hatua kimaendeleo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment