Image
Image

Mwanaharakati na mwandishi wa vitabu maarufu Zanzibar awashauri Rais Shein na Maalim Seif.

Mwanaharakati na mwandishi wa vitabu maarufu Zanzibar, Amir Ali Mohamed, amesema pamoja na kuvurugika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado ina umuhimu mkubwa katika kujenga amani na umoja wa kitaifa visiwani humo, hivyo hainabudi kudumishwa.

Alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa,akizungumzia viongozi wa kisiasa na umuhimu wa kulinda amani na umoja wa kitaifa kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa Zanzibar.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeleta mafanikio makubwa kwa watu wa Zanzibar kisiasa na kiuchumi na kufanikiwa kupunguza siasa za chuki na ubaguzi zilizokua zimewekwa na wakoloni kwa madhumuni ya kuwagawa ili kuwatawala.

“Maisha bora kwa wakulima wa zao la karafuu yameanza kuonekana baada ya serikali ya pamoja kufanikiwa kuinua bei ya zao hilo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein,” alisema na kuongeza:

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeleta utulivu kwa miaka mitano yote ilipokua inafanyakazi.”

Amir ambaye pia ni Katibu Jumuiya ya Sanaa na Utamaduni Zanzibar, alisema kutokana na kumalizika kwa siasa za chuki na uhasama Zanzibar, milango ya kiuchumi imefunguka kwa wawekezaji wa kigeni na wazalendo kuanza kuwekeza katika sekta za viwanda na huduma za tiba visiwani humo.

“Nawasihi viongozi wetu wa kisiasa wasiweke sana maslahi binafsi mbele ya kupata nyadhifa kubwa serikalini,  tuweke mbele maslahi ya taifa na wananchi, huko ndiko kupevuka kisiasa, tujengee vizazi vijavyo nchi bora na yenye utulivu wa kudumu,” alisema.

Hata hivyo, Amir alisema ili malengo hayo yaweze kufikiwa, wakati umefika kwa viongozi wa kisiasa kujenga uvumilivu wa kisiasa ikiwamo kutupilia mbali siasa chuki na historia.

“Nyinyi viongozi wetu, akiwa ni Dk. Ali Mohamed Shein, Maalim Seif Sharif Hamad, Balozi Seif Iddi tunawaomba mkutane tena ili mwendeleze Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatufaa Wazanzibari, msichoke kwani jinamizi la ukoloni lipo nyuma, wekeni mgawo wa madaraka ili pande zote ziridhike muongoze Zanzibar kwenye maendeleo na matumaini makubwa kwa wananchi wake,” aliongeza kusema katika waraka wake huo wa kurasa sita kwa vyombo vya habari.

Zanzibar imeingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo kwa kile alichoeleza kugubikwa na kasoro nyingi ikiwamo udanganyifu.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment