Rais wa Marekani Barack Obama amempongeza rais wa Myanmar Thein Sein kwa
uchaguzi wa kihistoria, uliokipa ushindi chama cha Aung San Suu Kyi.
Katika kura zilizohesabiwa chama hicho kimepata asilimia 85.
Msemaji wa Serikali ya Myanmar ambaye pia ni waziri wa habari wa nchi
hiyo Ye Htut ambaye ametangaza pongezi za rais Obama, amesema rais huyo
wa Marekani amesifu jinsi uchaguzi wa Jumapili nchini ulivyokuwa huru na
wa kuaminika.
Ikiwa matokeo kamili ya uchaguzi huo yataendelea katika mkondo wa yale
yaliyokwishatangazwa, Suu Kyi na chama chake cha National League for
Demokracy, NDL ataupiga kumbo utawala wa majenerali wa kijeshi
walioitawala nchi hiyo hadi rais wa sasa Thein Sein alipoanzisha
mabadiliko makubwa ya kidemokrasia miaka minne iliyopita.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Myanmar, rais Obama ameahidi kuendeleza ushirikiano na serikali ya nchi hiyo.
Mafanikio ya sera za nje za Obama.
Rais Obama aliizuru Myanmar mara mbili katika kipindi cha miaka 3
iliyopita, akiwa na matumaini kwamba mabadiliko ya kidemokrasia katika
taifa hilo yatakuwa mafaniko ya kidiplomasia katika utawala wake.
Tayari rais Thein Sein na Mkuu wa jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing
wameutambua ushindi wa Suu Kyi, na wamempongeza kwa ushindi wake katika
uchaguzi huo wa kwanza huru kuwahi kuitishwa baada ya kupita miaka 25.
Viongozi hao wawili hali kadhalika wameelezea utayarifu wao wa kuheshimu
matokeo, na kukubali pendekezo la Aung San Suu Kyi kufanyika mazungumzo
ya maridhiano ya kitaifa, lakini bado vyama havijakubaliana juu ya mada
ya mazungumzo hayo.
Bado wamyanmar hawajaamini
Hata hivyo, mashaka yanabakia miongoni mwa wananchi wa Myanmar, kama
mara hii wanajeshi watakubali kukabidhi madaraka kwa mshindi, kama
anavyoeleza mmoja wao, Maung Shwe:
''Nina mashaka kidogo kuhusu kukabidhi madaraka, kwa sababu hali kama
hii ilishatokea hapa katika uchaguzi wa 1990'' amesema Shwe na kuongeza
kuwa bado kumbukumbu hiyo wanayo na haitaondoka katika mawazo yao.
Tangazo la serikali limejaribu kuyaondoa mashaka hayo, likisema
itayaheshimu maamuzi ya raia, na itakabidhi madaraka kwa muda uliowekwa.
Hali kadhalika, tangazo hilo limeuhakikishia umma kwamba rais wa nchi
hiyo atashirikiana na watu wengine katika kuhakikisha usalama na
utengamano wa nchi baada ya uchaguzi huu.
Lakini jeshi nchini Myanmar linaendela kuwa na ushawishi mkubwa katika
siasa za nchi hiyo, limetengewa asilimia 25 ya viti vyote bungeni kwa
mujibu wa katiba. Juu ya hayo kamanda mkuu wa jeshi hilo anaachiwa uwezo
wa kuwateuwa mawaziri muhimu watatu, wakiwemo wa ulinzi, mambo ya ndani
na ilinzi wa mipaka ya nchi.
Udhibiti wa wizara ya ndani unalipa jeshi uwezo wa kusimamia shughuli za
utawala wa ndani, hali ambayo ni changamoto kwa Aung San Suu Kyi katika
kutekeleza sera za chama chake. Bado Suu Kyi hajatoa maelezo kuhusu
namna atakavyoishughulikia changamoto hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment