Image
Image

Suluhu ya mgogoro Zanzibar li[pewe kipaumbele.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar yalifutwa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi huo pamoja na matokeo yake yote.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya madai ya kubainika kuwapo na kasoro nyingi za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Baada kutangazwa majimbo 31 kati ya 54, ZEC ilidai kulikuwa na kasoro nyingi zilizoufanya uchaguzi huo kutokuwa huru na kuzingatia haki.
Kasoro nyingine zilizodaiwa kujitokeza ni kura kuongezeka katika baadhi ya majimbo kisiwani Pemba tofauti na idadi ya walioandikishwa kwenye Daftari la Wapigakura,  na pia madai ya baadhi ya makamishna wa ZEC kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati na kupigana.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha  alidai kuwa katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia kura yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo alichodai ni kinyume na sheria za uchaguzi.
Aidha kuna madai ya kuwapo kwa taarifa ya baadhi ya mawakala wa wagombea kufukuzwa, hali ambayo ilisababisha kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, na ambaye pia ndiye mgombea nafasi ya u-rais kupitia CUF, anadai kuwa ni mshindi wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo huko Zanzibar.
Maalim Seif ameitahadharisha ZEC kuwa kama Jecha ataendelea na msimamo wake wa kuufuta uchaguzi huo na kupuuza maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura, viongozi wa CUF watajiweka kando kutowazuia wananchi watakapotaka kudai haki yao.
Tamko hilo ni ishara tosha za kuwepo dalili za kutoweka kwa amani visiwani Zanzibar, hatua za dharura zinatakiwa zifanyike ili kuinusuru Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isiingie katika vurugu za kisiasa zinazoweza kuathiri mshikamano wa Watanzania na amani.
Tunaamini vyombo vya sheria vinaendelea kuwasiliana na viongozi wakuu wanaohusika katika sakata hili ili kupata ufumbuzi wa mtafaruku huu wa Kikatiba.
Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alikwenda visiwani Zanzibar ili kutafuta suluhu ya sintofahamu iliyojitokeza baina ya vyama vya CCM na CUF baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu na matokeo yake.
Jaji Mutungi amekiri kuwa upo umuhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar kukutana ili kutatua mzozo wa kisiasa uliojitokeza, na kwamba hakuna haja ya kuruhusu migogoro ambayo inaweza kusababisha kutoweka kwa amani nchini.
Jaji Mutungi na ujumbe wake waliweka dhamira ya kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa madhumuni ya kupata ufumbuzi wa tofauti zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu visiwani humo.
 Hatua hizi za awali za kusuluhisha mgogoro huu wa Zanzibar ni lazima ziungwe mkono na viongozi waandamizi wa kila chama nchini, ni kutokana na ushawishi walio nao pamoja na ushirikiano wa karibu miongoni mwao ambao utasaidia kutuliza mtafaruku wa hali ya kisiasa Zanzibar.
Ingawa baadhi ya vyama kama ADC kimekubali kushiriki uchaguzi wa marudio kwa kadri itakavyopangwa na ZEC, bado kuna haja ya kuangalia kwa umakini mahusiano ya vyama vikubwa vya CCM na CUF visiwani humo kwani ndivyo vyenye wafuasi wengi wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa.
Tunaamini mzozo huu utamalizika kwa mazungumzo yenye maafikiano ya kweli, tunawasihi viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa Zanzibar kuwa na subira ili taifa lisiingie kwenye misukosuko isiyokuwa ya lazima.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment