Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imevunja rekodi baada ya
kukusanya Sh.trilioni 1.3 kwa Novemba.
Hii nii baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia
madarakani na kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa TRA na pia kudhibiti
ukusanyaji wa mapato.
Jambo hili ni la kupongezwa kutokana na ukweli kwa miaka
mingi viongozi walijenga dhana kuwa Tanzania ni nchi maskini na ilikuwa haina
uwezo wa kujitegemea.
Matokeo yake, wananchi wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa
kwa kuaminishwa kuwa nchi yao ni maskini na ilipaswa kutegemea misaada ya nje.
Na hiyo ndiyo ikawa staili ya viongozi wengi kuhalalisha
safari za kwenda nchi za nje ili kusaka misaada ‘eti’ kwa kuwa nchi yetu ni
maskini!
TRA imepata mafanikio haya baada ya serikali kubana eneo
moja tu la bandari katika kuhakikisha watu wanalipa kodi kihalali.
Mamlaka hiyo ilivunja rekodi ya kukusanya mapato ya awamu ya
nne, ambayo kiwango chake cha juu kilikuwa Sh. bilioni 800 hadi bilioni 900.
Tunaupongeza uongozi wa TRA na serikali katika kuhakikisha
kuwa kiwango kikubwa cha mapato kinakusanywa.
Serikali imepanga fedha zilizokusanywa kuelekezwa katika
utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli, ya kutoa elimu bure.
Katika kutekeleza mpango huo wa elimu bure, serikali
imetenga Sh. bilioni 131 ambazo zitatakiwa kupelekwa shule mbalimbali. Mpango
huo wa kutoa elimu bure unahusisha utoaji wa vitabu na kugharimia chakula.
Tunaamini katika serikali na TRA wakiendeleza kasi hii ya
kukusanya mapato, kuna uwezekano kabisa wa kuifanya nchi yetu kujitegemea.
Waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere na hayati Abeid Karume, ndoto yao kubwa ilikuwa kuifanya nchi yetu
ijitegemee.
Ni kwa msingi huo, Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika
kilimo na ujenzi wa viwanda kwa kuamini vingechochea maendeleo na kuifanya nchi
yetu kutotegemea misaada kutoka nje.
Hayati Karume naye alitumia zao la karafuu kuiendeleza
Zanzibar, na hivyo akaanza mradi wa ujenzi wa nyumba kwa watu wake na
miundombinu.
Bahati mbaya katika miaka ya karibuni, viongozi wengi
walijielekeza zaidi katika kujineemesha.
Si jambo la ajabu kusikia viongozi wakitumia mabilioni ya
fedha kwa kisingizio cha kwenda kusaka fedha za misaada nchi za nje badala ya
kuandaa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Kama ambavyo, Rais Magufuli amesema kuwa anaamini mapato
haya yataongezeka zaidi kwa kuwa jambo hili linawezekana. Mathalani, serikali
ikianza kubana fedha zinazokusanywa na halmashauri mbalimbali nchini ina maana
mapato ya serikali yatapanda.
Bado hapo hatujazungumzia kampuni mbalimbali za uwekezaji
ambazo hupewa misamaha ya kodi.
Pia kuna maeneo mengine ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kama
gesi na madini. Kwa mafanikio haya ya muda mfupi ya serikali ya awamu ya tano,
kunadhihirisha kuwa umaskini wa Tanzania unachangiwa zaidi na mipango mibovu.
Hakuna maajabu yoyote kwa nchi kupiga hatua kimaendeleo kwani vitu
vinavyohitajika ni watu kujituma, nidhamu na dhamira thabiti.
Tunaamini serikali ya awamu ya tano ikiendelea na kasi hii,
itafanikiwa katika kipindi kifupi kutimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere ya Tanzania
kujitegemea na kuachana na kuomba omba misaada.
0 comments:
Post a Comment