Mechi ya mpira wa kandanda ya klabu za nyumbani
itapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga kwa mara ya kwanza katika historia
ya Somalia leo.
Fainali ya kombe la Jenerali Da'ud kati ya timu ya
Jeshi la Somalia Horseed na ile ya idara ya Polisi Heegan itaonyeshwa moja kwa
moja na runinga ya taifa ya Somalia.
Rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Somalia,
Abdiqani Said Arab, ametaja hatua hiyo kama historia kwa taifa hilo na afueni
kwa ukuaji wa mchezo huo nchini humo.
Somalia ingali inajaribu kujinasua kufuatia vita vya
wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.
''Tulikuwa na ndoto kuwa siku moja mechi zetu
zitaonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga, na huu ni mwanzo wa ndoto hiyo
kutimia',” anasema Said Arab.
Anaongeza kusema kuwa mechi hiyo ni jaribio lao la
kwanza na ikiwa litafanikiwa, watajaribu kuonyesha mechi nyingine miezi ijayo.
Michuano ya kuwania kombe la Jenerali Da'ud ndiyo ya
pili katika michezo kwa kuvutia mashabiki wengi nchini humo.
Shindano hilo hufanyika kila mwaka na limepewa jina
hilo kutokana na mwanzilishi wa Jeshi la Somalia, Jenerali Da'ud Abdulle Hersi.
Jenerali Da’ud, alifariki mwaka wa 1965 na serikali
ya Somalia imekuwa ikiandaa na kufadhili kombe hilo la soka tangu mwaka wa
1972.
0 comments:
Post a Comment