Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atawahutubia wanachama wa CDU katika
juhudi za kuwaunganisha baada ya kuwepo tofauti miongoni mwao kutokana
na msimamo wake wa kuwapokea maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani.
Kongamano la siku mbili la chama cha CDU linalofaniyka katika mji wa
kusini magharibi mwa Ujerumani wa Karslruhe unalenga kufikia mtizamo wa
pamoja kuhusiana na suala la wahamiaji baada ya wiki kadhaa za kuvutana
miongoni mwa wanachama wa chama hicho na ikiwa imesalia miezi mitatu tu
kabla ya uchaguzi wa majimbo kadhaa muhimu.
Ujerumani inatarajiwa kupokea wahamiaji milioni moja ifikapo mwishoni
mwa mwaka huu, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kupokewa na nchi ya Ulaya.
Kuwasili kwa wahamiaji wapya kumemfanya Kansela wa Ujerumani Angela
Merkel kushinikizwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na mzozo huo
hasa ndani ya chama chake mwenyewe.
Wahamiaji ndiyo mada kuu
Zaidi ya wajumbe 1,000 watamsikiliza Merkel akitetea sera zake kuhusu
suala hilo la wahamiaji ambapo ametakiwa kuchukua hatua madhubuti
kupunguza mmiminiko wa wahamiaji lakini wakati huo huo kuacha milango
wazi kwa wanaotoroka vita na machafuko nchini mwao.
Hapo jana Merkel alisema bila shaka watakuwa na mjadala wa kina kuhusu
suala hilo katika kongamano hilo la CDU kwani ndilo jambo ambalo
Ujerumani nzima inalizungumzia.
Kansela huyo wa Ujerumani hata hivyo amesema kwake ni muhimu sana kusema
kuwa watatekeleza wajibu wao wa kibinadamu na wajibu wao kwa Ulaya.
Merkel na chama chake ambacho amekiongoza kwa miaka 15 watatoa azimio
kuhusu suala hilo la mzozo wa wahamaji ambalo litapigiwa kura baada ya
hotuba yake ambayo wachambuzi wanasema itakuwa kama kura ya maoni kuhusu
utawala wake.
Huku wahamiaji na wakimbizi wakizidi kumiminika Ujerumani hata wakati
huu wa msimu wa baridi kali,wajerumani wanamtaka Merkel mwenye umri wa
miaka 61 kutoa muongozo bayana kuhusu ni namna gani atalishughulikia
suala hilo.
CDU Bado imara
Wanachama wa CDU wanatiwa wasiwasi na msimamo wa kiongozi wao huku
chaguzi za majimbo matatu muhimu zikitrajiwa mwezi Machi mwakani ambapo
kutokana na manung'uniko miongoni mwa raia huenda chama cha mrengo wa
kulia cha AFD kikapata uungwaji mkono zaidi ambacho kulingana na kura za
maoni kinaungwa mkono kwa asilimia 10.
Hata hivyo chama cha CDU bado kinaongoza katika uungwaji mkono miongoni
mwa umma kwa asilimia39 huku chama mshirika wake serikalini cha SPD
kikifuata kwa asilimia 24.
Uamuzi pia unatarajiwa mwaka ujao iwapo Merkel ndiye atakayepeperusha
bendera ya chama cha CDU katika uchaguzi mkuu mwaka 2017. Merkel kufikia
sasa hana mpinzani ndani ya chama chake huku wakosoaji wake wakikiri
kuwa kufikia sasa anasalia kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi
kuweza kugombea tena wadhifa wa Kansela wa Ujerumani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment