MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Bitun Msangi,ametangaza
kufuta ziara za mafunzo kwa madiwani wa halmashauri hiyo na badala yake
amewataka waende kujifunza vijijini.
Onyo hilo amelitoa alipokuwa akizungumza na
wananchi wa vijiji vya Mseta, Manhweta na Mseta Bondeni Kata ya
Chamkoroma, wakati akikabidhi vyeti na kombe kwa wananchi waliofanya
vizuri katika utunzaji wa mazingira ikiwamo ujengaji wa vyoo vya kisasa .
Alisema badala ya kufanya ziara hizo katika halmashauri nyingine,
watatakiwa kwenda kujifunza katika vijiji vyao ambako kuna changamoto
nyingi na watajadiliana jinsi ya kuzitatua.
“Mfano ulio hai ni hapa kwenye kata hii ambapo kama madiwani wakiamua
kuja kujifunza wanaweza wakapata elimu ya kuwaelimisha wananchi wa kata
nyingine ambazo mazingira ya usafi bado ni dhaifu,” alisema DC Msangi.
Alisema wananchi wa vijiji vya kata hiyo wameweza kunufaika na mpango
wa vyoo vya kisasa kwa asilimia 100 kwa kila kaya kuwa na choo cha
kisasa, ikiwemo kibuyu chirizi, shimo la taka na kichanja cha kuwekea
vyombo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango wa Mradi kutoka shirika la
UMATA, Nyomzobe Malimi, alisema vijiji hivyo vimefanikiwa katika
ujenzi wa vyoo ikiwemo uwekaji wa vibuyu mchirizo kwa aslimia 100
tofauti na vijiji vingine vinavyofadhiliwa.
Alisema mradi huo umewekewa mikakati ya miaka mitano kuhakikisha
unawawezesha zaidi ya watu milioni moja katika wilaya tatu wanafikiwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment