Image
Image

Ndali chako kuanza na shule za serikali kujua sababu za matokeo mabaya.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako, amesema atafuatilia shule za Serikali ili kujua sababu za kufanya vibaya katika mitihani yao. Dk Ndalichako ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), amesema hayo jana baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo.
“Kwa kuwa lengo langu ni kuona elimu bora inatolewa, nitafuatilia kujua sababu ya shule maalumu za Serikali kushuka kiwango chake katika ufaulu wa mitihani,” alisema. Kwa mujibu wa Dk Ndalichako, shule hizo za Serikali hasa za vipaji maalum, ndizo awali kila mwanafunzi alipenda kwenda kusoma tofauti na sasa ndio maana anataka kujua kulikoni.
Shule hizo ni pamoja na Mzumbe, Ilboru, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Kilakala na Msalato. Ada holela, kukaa chini Kuhusu upandaji holela wa ada za shule binafsi, Dk Ndalichako alisema atapambana na vyuo vikuu na shule binafsi, zinazofanya ujanjaujanja wa kupandisha ada tofauti na ile iliyoandikwa kwenye barua za kuwaita wanafunzi, jambo linalosababisha usumbufu kwa wazazi.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha Tanzania inatoa elimu bora kwa wahitimu wa vyuoni na sekondari, itakayowawezesha kukidhi soko la ajira la kimataifa. Pamoja na ubora huo, Dk Ndalichako alisema ataangalia uwepo wa miundombinu kwa wanafunzi wa kuanzia shule ya msingi na sekondari, ambako alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi wanaketi chini na wengine wana matatizo ya mashimo ya vyoo.
“Inakuwaje shule yenye maelfu ya wanafunzi watumie shimo moja la choo, haya na mambo mengine yanakwaza wanafunzi wasipende shule na wengine wakatize masomo yao. “Tunataka kuandaa mwanasayansi, hivi kweli mwanafunzi anayeketi chini anaweza kuwa mtaalamu mzuri wa sayansi? Ni lazima tuwezeshe shule zetu ziwe na miundombinu rafiki kwa wanafunzi,” alisema Dk Ndalichako.
Pia alisema atashughulika na tatizo la baadhi ya vyuo kutoa kozi zinazoenda kinyume na ithibati walizopewa na mamlaka za elimu, jambo linalofanya wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo hivyo kutotambuliwa na waajiri.
Profesa Mbarawa Kwa upande wake, Profesa Makame Mbarawa, ambaye amevaa viatu vya Dk Magufuli kwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alimshukuru Rais kwa kumwamini ili avae viatu vyake.
Pia, alikiri hatakuwa kama alivyokuwa mtangulizi wake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo uzoefu wa kazi ndani ya wizara husika. “Kiukweli mtangulizi wangu ni mtaalamu zaidi katika wizara hii na alikaa muda mrefu, hivyo siamini kama nitaweza kuwa kama yeye, ila nitajifunza kwake zaidi na ninategemea ushauri wake katika kutekeleza majukumu yangu mapya,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ameingia kwenye wizara hiyo, akiamini kuwa nchi bila kuwa na miundombinu madhubuti, haiwezi kufikia malengo yake, hivyo mkakati wa wizara yake ni kuunganisha nchi kwa barabara za lami kati ya makao makuu ya wilaya na wilaya, ili kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2025.
Alisema anatambua kwamba kuna miradi ya barabara zenye urefu wa kilometa 3,000, ambazo tayari makandarasi wanaendelea na ujenzi, hivyo atazisimamia ili zikamilike kwa wakati. Mbali na hiyo, pia alisema kuna barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 4,600, ambazo makandarasi wamepatikana na sasa ujenzi wake unasubiri kuanza; “Hizo nazo naahidi kuwa tutazijenga ndani ya miaka mitano,” alisema.
Alisema miradi mingine ambayo Wizara ya Ujenzi chini ya Dk Magufuli imejipangia kuijenga miaka ijayo, yeye ataenda kusimamia pamoja na sera za chama kuhakikisha kuwa ndoto ya ujenzi wa barabara hizo pia unakamilika.
Kwa upande wa reli, alisema kumekuwapo mpango wa kujenga Reli ya Kati ili iwe ya kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa na alisema anaamini Serikali imefikia pazuri na muda wowote ujenzi wake utaanza.
“Muda umefika sasa wa reli hiyo ianze kujengwa na Watanzania watarajie kuiona ili mizigo isafirishwe kwa treni na badala ya barabara, binafsi naamini kipindi hiki reli itaanza kujengwa,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wa sekta ya uchukuzi, alisema kuna fursa nyingi ambazo Taifa likitumia vizuri, itakuwa rahisi nchi kutekeleza lengo lake la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment