WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amelitaka
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (Dawasco), kufikisha maji
kwa wateja milioni moja hadi kufikia Juni mwaka ujao.
Mbarawa alimtaka Mkurugenzi wa Dawasco, Cyprian Luhemeja kuongeza
makadirio waliyokuwa wamejiwekea kwa kuongeza wateja kutoka 148,000
waliopo kwenye bili hadi kufikia milioni moja.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana katika ziara yake ya kwanza tangu
alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa wiki ambapo alisema
uzalishaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam unategemea mitambo ya
Ruvu Juu, Ruvu Chini pamoja na ule wa Mtoni.
“Naamini pindi tutakapofanya mazungumzo ya kina tutafikisha kiasi
hicho cha wateja hiyo Juni mwakani na hilo mtalipima kwenye tathimini
tutakapokutana Februari,” alisema Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine waziri huyo alitoa wito kwa Dawasco kuanza
mchakato wa kutumia mita za mfumo wa kulipia kabla kama inavyofanyika
kwa simu na umeme.
“Njia hii naamini itasaidia kuwabana wakwepaji wa kulipa na hivyo
kusaidia Dawasco kujipatia mapato ya kutosha,” alisema Mbarawa.
Alitoa wito kwa Mkurugenzi wa Dawasa, Archard Mutalemwa kuhakikisha
wanaweka miundombinu bora ili kuokoa upotevu wa maji ili kuboresha
huduma ya kuongezeka kwa wateja walio kwenye mfumo wa bili watakaofikia
milioni moja.
Akizungumzia kuhusu mipango yao, Mkurugenzi wa Dawasco, Luhemeja
alisema wanaamini idadi hiyo itafikiwa huku akisema hadi sasa katika
jiji la Dar es Salaam wateja wamefikia asilimia 68 wanaopata maji kwa
uhakika.
Alisema hadi kufikia Februari wataweza kuvuna maji mengi kutoka mita
za ujazo 300,000 hadi kufikia mita za ujazo 756,000 zitakazohudumia
wateja wapya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment