Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John
Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa Takukuru Dr Edward Hosea ambapo nafasi yake
itakaimiwa na Valentino Mlowoka kutokana na kutoridhishwa na namna taasisi hiyo
ilivyokuwa inatekeleza wajibu wake katika kudhibiti na kupambana na rushwa hapa
nchini.
Hatua hiyo ya rais Dr John Pombe Magufuli iliyotolewa
na katibu mkuu kiongozi balozi Ombeni Sefue Ikulu jijini Dar es Salaam imekuja
kufuatia dhamira ya dhati ya rais Dr Magufuli ya kupambana na rushwa na kwamba
kutokana na uwepo wa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya kukithiri kwa
suala la rushwa katika mamlaka ya Bandari Tanzania na mamlaka ya mapato
Tanzania TRA bila ya kuchukuliwa hatua zozote na mkurugenzi huyo wa Takukuru
imemfanya rais Dr Magufuli kuchukua hatua.
Ikumbukwe pia mara baada ya rais Dr Magufuli
kuapishwa na kuingia ofisini alipiga marufuku safari za nje ya nchi bila ya
kibali cha rais, makamu wa rais ama katibu mkuu kiongozi baadhi ya watumishi
wakiwemo watumishi wanne wa Takukuru walioomba kibali cha kusafiri nje ya nchi
na kukataliwa lakini wakaamua kusafiri rais amewachukulia hatua za kinidhamu.
Aidha katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue
ametahadharisha kuwa agizo hilo la rais si la mzaha na kutoa maagizo kwa
makatibu wengine wakuu.
0 comments:
Post a Comment