Image
Image

Magufuli:Ahadi ya kutoa elimu Bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne iko palepele.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ni lazima itekelezwe huku akimpongeza kaimu kamishna mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa kodi.

Rais Dr Magufuli ameyasema hayo Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kwa mara ya kwanza mamlaka ya mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi Trilioni moja nukta tatu ambazo baadhi zitasaidia kutoa elimu bure huku akitoa angalizo kwa walimu na watendaji watakaotumi visivyo fedha.

Amesema kuwa fedha hizo ambazo zitatumika kwaajili ya kuoa elimu bure anataka zitumike ipasavyo na kusema kuwa watakao tumia vibaya atakula nao sahani moja kwani hakutahitajika mchango wowote katika shule zitakazoanza mchakato huo wa elimu bure.

Siku za usoni WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi ilitoa waraka wa elimu kuhusu elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais John Magufuli.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo kuwa ni
- Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Diamond (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Iringa (Iringa) na
- Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine ni
- Shule ya Msingi Angaza (Mbeya);
- Shule ya Msingi Nuru (Mbeya);
- Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma);
- Shule ya Msingi Tanga (Tanga);
- Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na
- Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu sawa na shule za binafsi.
Katika waraka huo, Wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara hiyo, TAMISEMI, Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi
Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
Katika waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo unaielekeza wizara hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimumsingi bila malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi, kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni za kugharimia wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu maalumu kwa kuwapatia chakula yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo mitatu kwa wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule
Waraka huo unawataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina ya vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, sare za michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia wanafunzi ili wazazi wanunue wenyewe.
Pia wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za Serikali na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na mahitaji mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule
Wizara katika waraka huo inataka kamati za shule kufuatilia na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze kuleta tija; kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.
Kuwashirikisha wazazi, walezi, walimu na wanafunzi katika maamuzi na maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule kwa ujumla.
Pia waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni kusimamia sera na miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi ambao ndio walengwa wakuu wa utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo shule katika kipindi chote cha masomo.



Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment