Raia wa Rwanda wameanza kufika vituoni kushiriki
kwenye kura ya maoni ya marekebisho ya katiba, ambayo yakiidhinishwa
yatamruhusu Rais Paul Kagame kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa asubuhi na
mapema, huku watu 6 milioni wakitarajiwa kupiga kura. Bw Kagame anatarajiwa
kupiga kura katika kituo cha Rugunga mjini Kigali.
Mabadiliko hayo yakiidhinishwa, huenda yakamuwezesha
Bw Kagame kusalia madarakani hadi 2034.
Marekani imetoa wito kwa Bw Kagame kuonyesha
uzalendo na kuondoka madarakani muda wake ukimalizika mwaka 2017.
Lakini kiongozi huyo ameyashambulia mataifa
yanayotoa wito huo, akisema yanaingilia maswala ya ndani ya taifa hilo la
Afrika Mashariki.
Mwezi uliopita, Bunge la Seneti nchini Rwanda
liliidhinisha marekebisho hayo na kupisha kuandaliwa kwa kura ya maoni.
Bw Kagame atakuwa radhi kuwania urais kwa muhula
mwingine wa miaka 2017 marekebisho yakiidhinishwa.
Hata ingawa marekebisho hayo yanapunguza muda wa
muhula wa rais kutoka miaka saba hadi miaka mitano, na kudumisha muda wa mihula
miwili, sheria hiyo haitaanza kutekelezwa hadi mwaka 2024.
Hii ina maana Bw Kagame atakuwa huru kuwania urais
kwa mihula mingine miwili ya miaka mitano mitano.
0 comments:
Post a Comment