Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa jana Ijumaa
(18.12.2015) kwa kauli moja limepitisha azimio linaloidhinisha muongozo wa
kimataifa kwa ajili ya hatua za amani nchini Syria .
Hii ikiwa ni hatua ya kipekee ya iliyoonesha umoja
miongoni mwa mataifa makubwa katika mzozo ambao umesababisha kupotea kwa maisha
ya watu zaidi ya robo milioni.
Azimio hilo linatoa ridhaa kwa mpango uliojadiliwa hapo
kabla na Umoja wa Mataifa mjini Vienna ambao unatoa wito wa kusitishwa
mapigano, mazungumzo baina ya setikali ya Syria na upinzani, na muda wa miaka
miwili ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa Kitaifa na kisha kufanya uchaguzi.
Mkwamo bado upo
Lakini vikwazo katika kumaliza karibu miaka mitano ya
vita vya wenyewe kwa wenyewe bado vinaendelea kuleta mkwamo, ambapo hakuna
upande katika mzozo huo ambao unaweza kupata ushindi wa wazi kupitia njia za
kijeshi.
Licha ya makubaliano yao, mataifa makubwa yanatofautiana
mno juu ya nani huenda akawakilisha upinzani pamoja na hali ya baadaye ya rais
Bashar al-Assad.
"Baraza hili linatoa ujumbe wa wazi kwa wale wote
wanaohusika kwamba muda ni sasa wa kusitisha mauaji nchini Syria na kuweka
msingi kwa ajili ya serikali ambayo umma unaoteseka kwa muda mrefu katika nchi
hiyo iliyotumbukia katika mzozo unaweza kuiunga mkono," waziri wa mambo ya
kigeni wa Marekani John Kerry ameliambia baraza hilo lenye wanachama 15 baada
ya kura hiyo.
Azimio hilo pia linatoa wito kwa Umoja wa Mataifa
kuwasilisha katika baraza hilo uwezekano wa kuangalia usitishaji mapigano
katika muda wa mwezi mmoja.
Mazungumzo kati ya serikali ya Syria na upinzani
yanapaswa kuanza mapema Januari, azimio hilo limesema, licha ya kuwa Kerry
amesema katikati hadi mwisho wa Januari huenda ni muda muafaka zaidi. Pia
azimio hilo limeidhinisha mapambano zaidi dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola
la Kiislamu ambao wamekamata maeneo makubwa nchini Syria na nchi jirani ya
Iraq.
Azimio hilo limekuja baada ya Urusi na Marekani kufikia
makubaliano ya waraka. Mataifa hayo mawili yamekuwa na mtazamo tofauti
kuhusiana na kile kinachopaswa kutokea nchini Syria , ambako wanamgambo wa Dola
la Kiislamu wanadhibiti eneo kubwa ambalo serikali za mataifa ya magharibi
wanashuku limekuwa eneo linalotumiwa kwa mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya
mataifa ya magharibi na Urusi.
Mustakabali wa rais Assad bado haujajulikana
Kerry ameweka wazi kwamba kuna tofauti bado kuhusu hali
ya baadaye ya Assad , mshirika wa karibu wa Urusi na Iran ambae mataifa ya
magharibi yanataka aondoilewe, pamoja na suala la makundi gani ya Syria
yatakuwa na viti katika meza ya duara katika mazungumzo pamoja na serikali.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius
amesema mazungumzo baina ya serikali ya Syria na upinzani yatafanikiwa tu iwapo
kutakuwa na uhakikisho wa kweli kuhusiana na kuondoka kwa Assad.
Balozi wa Syria Bashar Ja'afari amesema serikali ya Assad
iko tayari kushiriki katika mazungumzo hayo kwa nia njema kabisa.
Makubaliano katika azimio hilo yamekuja baada ya mkutano
wa kile kinachofahamika kama kundi linalotoa usaidizi kwa Syria katika hoteli
ya Palace mjini New York.
Usitishaji wa mapigano
Muongozo kuhusu Syria , ambao pia unatoa wito kwa
usitishaji wa mapigano nchi nzima ambao utahusisha pia Dola la Kiislamu, Nusra
Front na baadhi ya makundi ya wanamgambo, yalifanyiwa kazi hapo kabla katika
duru mbili za mazungumzo katika ngazi ya mawaziri mjini Vienna.
Wanadiplomasia wamesema tatizo kubwa katika majadiliano
kuhusu azimio hilo yaliyohusisha wasi wasi wa Urusi na Iran juu ya vipi
kuliangalia kundi la makundi ya wapinzani ambao watajiunga na mazungumzo
yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na serikali ya Syria.
Javad zarif aliandika katika gazeti la Guardian siku ya
Ijumaa kwamba ni kitu cha kushangaza sana, kwamba wale ambao wamewanyima watu
wao wenyewe haki za msingi kabisa za demokrasia...sasa wamejitangaza kuwa
mabingwa wa demokrasia nchini Syria.
Mkutano wa Riyadh umekubaliana kuunda sekretariati yenye
wajumbe 34 kuangalia mazungumzo ya amani , na kamati hiyo pia itachagua watu
kutoka upande wa upinzani watakaoshiriki katika mazungumzo hayo.
0 comments:
Post a Comment